BOB OGOLLA |
Kocha Msaidizi wa
Gor Mahia, John Bobby Ogolla, amemruhusu mpachika mabao wake, Michael Olunga
kutua kuichezea Simba msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Olunga alikuwa
mwiba kwenye safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa inaongozwa na Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani wakati timu hizo zilipovaana katika mechi ya
kwanza ya Kombe la Kagame, iliyomalizika kwa Yanga kufungwa mabao 2-1, huku
mshambuliaji huyo akipachika moja.
BOB OGOLLA AKIWA NA BOSI WAKE WA ZAMANI, BOBBY WILLIAMS |
Mshambuliaji
huyo mwenye umbile kubwa, yupo kwenye orodha ya wachezaji wanaowaniwa na Simba
ambaye hivi sasa anaongoza kwenye orodha ya wafungaji katika michuano ya Kombe
la Kagame akiwa amepachika mabao matatu.
OLUNGA... |
Ogolla ambaye ni mwanasoka nyota wa zamani wa Gor Mahia pamoja na Harambee Stars alisema
wao kama viongozi hawawezi kumzuia mshambuliaji huyo kuondoka Gor Mahia,
kikubwa timu husika ifuate sheria zao.
Ogolla alisema
kikubwa wao wanapenda kuona wachezaji wao wanapata mafanikio ya kucheza soka la
kulipwa, hivyo yeye kama kiongozi anatoa baraka zake zote kwenda Simba au Yanga
kama zikimhitaji.
“Mimi kama kocha ninamruhusu Olunga kwenda
kuichezea Simba au hata Yanga kama ikimhitaji kwa ajili ya kumsajili kwa kuwa timu
hizo zilionyesha nia kubwa ya kumsajili.
“Kikubwa
nazishauri hizo timu zinazomhitaji kufuata sheria tulizojiwekea kama uongozi
katika kuhakikisha zinamsajili Olunga ambaye ni tegemeo kwenye timu yetu.
“Sisi kama timu
hatuwezi kumzuia mchezaji yeyote kwenda kuchezea timu nyingine kwa faida yake
mwenyewe ya kupata fedha nyingi zitakazoendesha maisha yake,” alisema Ogolla.
Mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga bao moja wakati timu yake ilipovaana na Yanga na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na juzi alifunga mabao mawili walipopata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMKM.
0 comments:
Post a Comment