DUWA SAID: TUNASUBIRI MUDA TU KIIZA ATUPE RAHA SIMBA SC
Duwa Said amesema ana imani na Kiiza atawapa raha wan Simba SC Jumamosi |
WINGA wa zamani wa Simba SC, Duwa Said ana imani kubwa na mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ kuelekea pambano dhidi ya mahasimu, Yanga SC mwishoni mwa wiki.
Simba SC na Yanga SC watamenyana Jumamosi wiki hii katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Na kuelekea mchezo huo, kinara wa mabao wa zamani wa Simba SC, Duwa amesema kwamba ana matumaini ya ushindi kwa timu yake na Kiiza ndiye atakuwa ‘muuwaji’.
“Kiiza ni mchezaji mzuri ambaye anajua kufunga. Anapokuwa uwanjani unaweza usimuone, lakini kwenye tukio ndiyo anaibuka anawainua watu. Nina imani naye sana kwamba atawaua Yanga,”amesema Duwa leo Dar es Salaam.
Duwa Said akiichezea Simba Veterans hivi karibuni |
Duwa ambaye yupo kwenye Kamati ya Ufundi ya Simba SC pamoja na beki wa zamani wa timu hiyo, Fikiri Magosso chini ya Mwenyekiti, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King KIbaden’ amesema Simba SC ipo vizuri kuelekea mchezo huo.
“Kwa ujumla timu nzima iko vizuri ila unapozungumzia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja Kiiza nina matumaini naye sana kwamba atawafunga YangaSC. Tunasubiri muda tu ufike atupe raha,”amesema.
Kiiza aliyesajiliwa msimu huu Simba SC baada ya kuwa nje kwa nusu mwaka kufuatia kutemwa na Yanga SC Desemba mwaka jana, kwa sasa ndiye tegemeo la mabao la Wekundu wa Msimbazi.
Kiiza amefunga katika kila mechi kwenye mechi tatu za mwanzo za Ligi Kuu, bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya African Sports, bao moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Mgambo na mabao yote matatu katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Kagera Sugar Jumapili.
Kwa sasa kikosi cha Simba SC kimeweka kambi kisiwani Unguja tangu jana kwa maandalizi ya mchezo huo ambao utaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV, wakati mahasimu wao nao, Yanga SC wamejichimbia kisiwani Pemba.
0 comments:
Post a Comment