MAWASILIANO

Phone. - +255 (717) 300 260 - +255 (787) 300 260

HABARI YA MUJINI

HABARI YA MUJINI
watu wa mpira

MAMBO MUHIMU, POPPE ANATAKIWA KUYAFANYA SIMBA SC…


poppe
Wakati alipotangaza kuwa Simba SC itapeleka barua kwa mahasimu wao, Yanga SC ili kumnunua kiungo-mshambulizi, Saimon Msuva, Zacharia Hans Poppe ameonekana kujiamini, lakini hilo linaweza kuwa sawa na kula chakula kilichowekwa sumu. Nilichokipenda kutoka kwa mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili ni namna alivyosema kuwa Simba itawasilisha maombi rasmi ya kumsaini Msuva.
Huu ndiyo usajili ambao siku zote wadau na mashabiki wa kandanda wamekuwa wakiutaka kuelekea mpira halisi wa kulipwa. Poppe amepiga hatua katika hilo, na hilo lisiwe kwa Msuva na Yanga tu, bali lihusishe wachezaji wote ambao Simba inafikiria kuwasaini kutoka klabu nyingine. Usajili mzuri wenye kufuata taratibu ni sehemu ya kutekeleza kauli mbiu ya mchezo wenyewe. Soka ni mchezo wa haki.
Wakati huu wa usajili wa dirisha dogo ukikaribia kuwa wazi, Simba ni miongoni mwa timu za ligi kuu Tanzania Bara ambazo zitalazimika kuingia sokoni kusaka wachezaji ambao wataimarisha timu hiyo iliyopata ushindi mara moja katika michezo saba msimu huu.
KUWASAJILI, NYOSSO, MWANTIKA, HARUNA BOBAN NA MGOSI…
Kumekuwa na vikao vya mara kwa mara katika siku za karibuni ambavyo kamati ya utendaji ya klabu na ile ya usajili wamekuwa wakifanya. Katika vikao hivyo, Simba inajadili uwezekano wa kuwarudisha katika timu hiyo wachezaji wake wa zamani, kiungo, Haruna Moshi ‘ Boban’ , mshambulizi Musa Hassan Mgosi, na walinzi, Salum Kanoni, Amir Maftah na Juma Nyosso. Pia timu inafikiria kumsaini mchezaji huru, mlinzi David Mwantika ambaye amemaliza mkataba wake na mabingwa wa Bara, Azam FC.
Haruna na Mwantika ni wachezaji ambao klabu ya Yanga inafikiria kuwasaini wakati wa usajili mdogo utakapokuwa wazi. Kama kamati ya Poppe itahitaji wachezaji wazoefu wenye ubora, Mgosi, Boban, Nyosso na Mwantika watafaa zaidi. Hawa kazi yao kubwa itakuwa ni kuwaongoza vijana wadogo kama, William Lucian, Mohammed Hussein, Miraj Adam, Abdi Banda, Hassan Isihaka, Abdallah Seseme, Jonas Mkude, Said Ndemla, Ibrahim Twaha, Ramadhani Singano, Elius Maguli.
Timu yenye balansi nzuri ya wastani wa umri hufanya vizuri. Ukichanganya uwepo wa Joseph Owino kama nahodha, Uhuru Suleimani, Amis Tambwe na Emmanuel Okwi, Simba watahitaji kuona wachezaji hao wakijituma ndani ya uwanja na kuisaidia timu kupata ushindi.
KUENDELEA KUMNG’ANG’ANIA, NDEMLA.
Baada ya kumuongezea mkataba, Mkude kamati ya utendaji na ile ya usajili wanapaswa kuhakikisha kiungo, Ndemla anaendelea kuichezea timu hiyo kwa muda mrefu. Ndemla ni kijana mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za kupenyeza hata akiwa katika umbali mrefu. Kocha wa Yanga, Marcio Maximo angependa kufanya kazi na mchezaji huyo, wakati pia Azam ikimtazama kama mchezaji anayeweza kuongeza kitu kipya katika timu yao. Yanga hawatakuwa tayari kumuuza Msuva kwa gharama yoyote katika timu za ndani, Simba pia wanapaswa kufanya hivyo kwa Ndemla mchezaji waliyemkomaza wenyewe.
KUISHI NA MATARAJIO…
Katika msimu wa 2009/10, Simba ilitwaa ubingwa pasipo kupoteza mchezo wowote, lakini mwaka mmoja baadaye sehemu kubwa ya wachezaji wa kikosi kile waliondolewa kwa sababu timu ilipoteza ubingwa ambao walikuwa na uwezo wa kuuchukua. Kukosa ushindi katika michezo mitatu kati ya minne ya mwisho katika msimu wa 2010/11 kulifanya Yanga kuchukua ubingwa kwa tofauti ya magoli.
Mgosi, Kaseja Juma, Kanoni, Hillal Echessa, Okwi walitajwa kama sababu kubwa ya kuanguka kwa timu hiyo msimu huo. Katika nyakati hizi za Poppe kama mwenyekiti wa kamati ya usajili, Simba imeshindwa kutamba licha ya usajili wa gharama kubwa ambao umeambatana na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha. Malengo na matarajio ya Simba msimu huu ni kutwaa ubingwa lakini siku zote matarajio huwa yanafika mwisho. Malengo makubwa ni kitu ambacho kitasukuma uwajibikaji wa kila mmoja klabuni, Poppe ana malengo makubwa lakini matarajio yanapofeli kuwe na staha na uvumilivu.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment