Na Saleh Ally
Kiungo wa pembeni wa Simba, Haruna Chanongo amebwaga manyanga na amesisitiza anataka kuondoka Simba huku taarifa zikithibitishwa kuwa Mtibwa Sugar, wako tayari kumpokea.
Chanongo yuko kwenye adhabu ya kusimamishwa kuichezea Simba kwa madai ya kucheza chini ya kiwango.
Taarifa zinaeleza Chanongo ameamua kuondoka, tayari ameueleza uongozi wa Simba kupitia meneja wake Jamal Kisongo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kisongo amesema tayari wamefanya mazungumzo na Simba imuachie Chanongo ambaye mkataba wake umebaki miezi sita tu ili aende akakipige Mtibwa Sugar.
“Simba nimezungumza nao kuhusiana na hilo, pia nimezungumza na Mtibwa Sugar ambao wako tayari kumpokea wakati wowote.
“Simba walisema wanaweza kumtoa Mtibwa Sugar kwa mkopo, mimi naona si sahihi. Nafikiri wamalizane tu, wamuache kijana akacheze. Naweza kusema Chanongo na Simba sasa basi,” alisema Kisongo na kuongeza.
“Mfano nimesikia Chanongo anataka kushushwa timu B, ikiwa Simba watafanya hivyo, hiyo ni dhambi kubwa. Huyo ni mchezaji wa timu ya taifa, huyu kijana ni masikini, bado anatafuta maisha, wasimfanyie hivyo, wamuache aondoke.
“Tatizo jingine kwenye familia ya huyu kijana wako watu Yanga, ndiyo inaleta shida. Kingine mimi pia ni mwanachama wa Yanga, basi imekuwa ndiyo tatizo. Basi wamuacha aende.
“Naweza kuwathibitishia Simba, Chanongo haendi Yanga. Wakati fulani Yanga walimpa milioni 30, nikazuia abaki Simba kwenye milioni 18, sababu tu nilitaka acheze. Wamwache huyu kijana, Simba na yeye, sasa basi inatosha” alisisitiza Kisongo.
0 comments:
Post a Comment