Na Saleh Ally
Mshambuliaji Mbwana Samatta anaondoka TP Mazembe ya DR Congo na hii si hadithi tena, Meneja wake, Jamal Kisongo amethibitisha hilo.
Awali, taarifa zilizolifikia gazeti hili na kufanya uchunguzi kwa wiki mbili, zilionyesha Samatta alikuwa anawaniwa na timu tatu za Ulaya, mbili kutoka nchini Ufaransa, tena zinashiriki ligi kuu nchini humo League 1.
Lakini jana, Meneja wake, Jamal Kisongo akathibitisha hilo kwa kusema tayari wamekuwa na mazungumzo marefu na uongozi wa TP Mazembe na mmiliki wake, bilionea Moise Katumbi amekubali kutoa ruhusa.
“Yalikuwa mazungumzo ya kina na marefu kiasi, lakini mwisho tumefikia mwafaka kwamba Samatta anaondoka TP Mazembe na anakwenda Ulaya.
“Kumekuwa na mtikisiko mkubwa ndani ya Mazembe, wengi hawakutaka aondoke. Lakini mkataba tulioingia mwanzo umembana Katumbi, amekubali Samatta aondoke Mazembe,” alisema Kasongo, akionyesha kujiamini.
Kasongo ambaye aliongozana na Samatta hadi Lubumbashi, DR Congo ambako aliingia mkataba na timu hiyo kwa mara ya kwanza, amesema hadi mwezi ujao kitakuwa kimeeleweka.
“Suala la kuwa majeruhi ndiyo limemchelewesha Samatta, lakini atalazimika kusubiri wiki tano alizopewa na daktari. Ndiyo maana nilizuia asirudi Mazembe, sikupenda atumike angeweza kuumia tena.
“Anatakiwa kwenda Ulaya, nisisitize si majaribio na wakala wake ni mtu mkubwa tu nchini Ufaransa, hivyo atalishughulikia suala hilo na kila kitu kinaenda vizuri.”
Kama ilivyo kwa kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, Samatta amekuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Mazembe na kumekuwa kuna ugumu kumng’oa Lubumbashi hadi juhudi za Kisongo zilipozaa matunda.
Alijiunga na Mazembe misimu mitatu iliyopita akitokea Simba ya Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment