Na Saleh Ally
GUMZO kubwa kwa sasa nchini ni wizi wa jumla ya shilingi bilioni 306 zilizoibiwa kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Uchotaji wa fedha kwenye akaunti hiyo, umetikisa nchi ikiwa ni pamoja na kuwataja vigogo mbalimbali wakiwemo wakubwa serikalini.
Ripoti hiyo imewataja hadi viongozi wa dini kuhusika katika mgawo wa uchotaji wa mamilioni ya fedha hizo ambazo ni mali ya wananchi.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac) ndiyo iliyofichua uchotwaji wa fedha hizo na kuweka mambo yote hadharani, moto bado unaendelea bungeni.
Katika sehemu ya taarifa ya Pac iliyosomwa na Mwenyekiti, Zitto Kabwe ilieleza namna watu walivyokwenda benki kugawana fedha hizo wakiwa na mifuko, maboksi na hata magunia.
Waliogawana fedha hizo kwa maboksi na magunia ni wale waliochota kiasi cha Sh bilioni 77. Hapo ndiyo tunarejea kwenye michezo.
Tanzania ni kati ya nchi yenye matatizo makubwa sana katika maendeleo ya michezo mbalimbali, acha tuutumie ule wa soka unaopendwa zaidi.
Kuna upungufu wa mambo mengi sana na hasa miundombinu ambayo ukosekanaji wake unafanya kuzorota kwa mchezo wa soka na maendeleo kwenda kwa mwendo wa kobe.
Hakuna vifaa na hasa viwanja, hata Ligi Kuu Bara imekuwa ikilalamikiwa kwa kuwa viwanja vinavyoweza kuchezewa na wachezaji wakaona wako kwenye uwanja sahihi ni vitatu tu.
Kimoja kinamilikiwa na serikali, ambacho ni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kingine ni mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kambarage, Shinyanga na kile cha Azam Complex, mali ya Azam FC, kiko Mbagala, Dar.
Ukirejea kwenye viwanja vingine vyote vilivyobaki, yaani Sokoine-Mbeya, Jamhuri-Morogoro, Mkwakwani-Tanga, Kaitaba-Kagera, vyote ni matatizo makubwa.
Kwa fedha Sh bilioni 306, Tanzania ingeweza kuwa na viwanja bora zaidi ya sita. Mfano kama ingeamua kutengeneza viwanja vyenye uwezo ukubwa kama ule wa Uhuru wa jijini Dar es Salaam, basi ingepata hata zaidi ya kumi.
Ukisema, serikali ingeamua kujenga viwanja kama vile ya Uwanja wa Taifa ambacho ni kati ya viwanja bora barani Afrika, basi ingeweza kujenga viwanja sita. Yaani vitano vya ukubwa kama huo Uwanja wa Taifa na mmoja kama Uwanja wa Uhuru.
Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam wenye uwezo wa kuingiza watu hadi 60,000 uliojengwa na kampuni ya Beijing Construction Engineering ya China kwa kitita cha Sh bilioni 56.4, serikali ya Tanzania ikiwa imetoa Sh bilioni 25 na Serikali ya China ikatoa kiasi kilichobaki.
Jiulize, nchi yenye viwanja saba kama Uwanja wa Taifa, kwa kuwa tayari Dar es Salaam kipo kimoja na mmoja mdogo wa kisasa kama ule wa Uhuru, kweli nchi itashindwa kupiga hatua kimichezo?
Kama fedha hizo zingetumika kujenga viwanja ambavyo vingekuwa katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga, Shinyanga, Morogoro na Dodoma (mfano). Hamasa ya maendeleo, ingepanda.
Kawaida hamasa ingekuwa juu, wengi wangependa kushiriki michezo na hasa watoto na vijana, ingekuwa rahisi timu mbalimbali kutoka nje kucheza hadi mikoani na kiwango cha soka nchini kingepanda kwa kuwa ushindani ungekuwa sahihi kwenye viwanja vinavyotakiwa.
Ingesaidia hamasa kwa michezo mingine kama mpira wa kikapu, ngumi na riadha kwa kuwa kungekuwa na sehemu nzuri ambayo ingetumika kwa ajili ya kuchezea.
Kwa viwanja kama hivyo, Tanzania ingekuwa ina uwezo wa kuandaa mashindano makubwa zaidi duniani kama Kombe la Dunia au Kombe la Mataifa Afrika bila ya hofu hata chembe kama utazungumzia masuala ya viwanja.
Fedha hizo ambazo mjadala wake bado unaendelea, zingeweza kutumika kwa maendeleo ya michezo au shughuli nyingine za kijamii, basi zingesaidia kupatikana kwa maendeleo makubwa kuliko ambavyo wachache wamegawana kwenye maboksi, magunia na mifuko ya sandarusi.
Hii inaonyesha kiasi gani kuna fedha zinatumika ovyo, ujanja mwingi na huenda huu ndiyo wakati wanasiasa na wafanyabiashara, kuionea huruma nchi yetu.
Fedha nyingi zinazoibiwa si kwenye Escrow pekee, hata kwenye kashfa lukuki za wizi zinazojitokeza, bado Tanzania ingeweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo, ingeondokana na utegemezi na kufika mbali kimaendeleo.
Fedha tunazo kibao, matumizi yake ndiyo tatizo na faida inakwenda kwa wachache huku watoka jasho wananchi wakiwa wanateseka.
Ingawa bado mjadala unaendelea bungeni na kwingineko, serikali ikisema si fedha za umma inaonekana haitakwepeka kwamba fedha hizo zimechotwa na wachache wasiofika hata idadi ya watu 40.
Halafu wamegawana mabilioni hayo rundo kwa ajili ya matumizi yao binafsi huku maslahi ya wengi katika taifa, yakiendelea kuteketea!
0 comments:
Post a Comment