MAWASILIANO

Phone. - +255 (717) 300 260 - +255 (787) 300 260

HABARI YA MUJINI

HABARI YA MUJINI
watu wa mpira

WAKATI HAUKUWA MWAFAKA MWAMBUSI KUONDOKA


Na Ben Shija
HESABU ya mechi saba za Ligi Kuu Bara ambazo Mbeya City imecheza kabla ya ligi hiyo kusimama, zinaonyesha hazijajipanga vizuri.


City imecheza mechi saba, imeshinda moja, sare mbili na kupoteza mechi nne, hivyo kuifanya ikusanye pointi tano tu na sasa inashikilia mkia ikiwa imezibeba timu 13 mgongoni!

Matokeo hayo yamewapa presha kubwa mashabiki, viongozi na wachezaji wa Mbeya City ambao kwa asilimia 95 wana kikosi kilekile cha msimu uliopita kilichoshika nafasi ya tatu.

Mbeya City ilishika nafasi ya tatu ikiwa ndiyo imepanda Ligi Kuu Bara, ikawa kigogo ya vigogo, ikazikomalia Yanga, Simba na Azam ingawa mzunguko wa pili ilionekana kushuka.

Mwendo mbaya, umesababisha kocha Juma Mwambusi ajiuzulu. Mwenyewe amehojiwa redioni na kusema kuwa ameachia ngazi, lakini uongozi bado unakwenda kulizungumzia, huenda wanjaribu kumtuliza.
Lakini kitu kibaya zaidi, Mwambusi amekuwa akishindwa kutoa ufafanuzi katika suala hilo, akikwepa kuzungumza na waandishi ingawa mara moja nimemsikia akithibitisha kujiondoa.

Uongozi umekuwa ukisisitiza kuwa, Mwambusi bado ni kocha wao, hivyo inachanganya ingawa kauli za kocha huyo zilionyesha zimejaa jazba.

Wakati anahojiwa na Redio One, Mwambusi alionyesha kukasirishwa na kitu na akazungumzia madai ya wachezaji wake kuwa wapo wanaoidai timu, yeye amekuwa akijaribu kuwashawishi wacheze kwa kujituma, lakini anaona sivyo.

Ukiangalia matumaini yaliyojengwa na furaha ya mashabiki wa Mbeya City, tayari waliipa timu yao daraja walilo Yanga, Simba, Azam FC kutokana na matokeo mazuri. Sasa wote wanaona kama wanasalitiwa, ndiyo maana wamekuwa hawataki kuamini.

Ukirudi kwa viongozi, ingawa ulikuwa ni msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara, waliona mambo ni rahisi, yanawezekana, mipangilio haina ugumu, ndiyo maana sasa wanashindwa kuidhibiti hali hiyo kwa urahisi.

Wachezaji wengi wa Mbeya City walikuwa ndiyo wanacheza ligi kwa mara ya kwanza. Pia waliona huenda kila kitu rahisi na wanaweza, sasa mambo yamekuwa tofauti.

Ukweli ni hivi, kama Mwambusi amepitisha uamuzi wa kuondoka na kwa mujibu ya nilivyomsikia redioni, basi nitamweleza mambo mawili.

Kwanza ameondoka mapema na pili hakuondoka kwa maana ya kwamba ameshindwa, lakini hakukubali kukaa ajaribu, badala yake amezisikiliza hisia zake, unaweza kusema Mwambusi amesusa.

Kiongozi au baba au mzazi, hukubali kubaki wakati laini yaani wa raha. Pia haiachi familia au timu kipindi cha shida, au cha matatizo. Mwambusi hakuwa tayari kulaumiwa, lakini alitakiwa kukubali ili atumie nguvu yake na uwezo wa msimu uliopita ili kuweka mambo sawa. Lawama haziishi dunia hii, hata ufanye mazuri kama malaika.

Ukiachana na Mwambusi, Mbeya City pia walijisahau na mtazamo wangu kuna mambo matatu yatakuwa ymechangia kuwapa ugumu, nitawaeleza kama zawadi yao. Wakiweza wanaweza kuyafanyia kazi.
Moja:
Wazungu wanasema ‘surprise’, yaani kitu cha kushtukiza. Hakuna aliyejua City ingekuwa imejiandaa kama ilivyokuwa msimu uliopita, mwanzo walionekana kama wanabahatisha, lakini wakaendelea kusonga.

Utaona mzunguko wa pili, watu wakatulia, wakaanza kupambana nao, ndiyo maana ilipoteza mechi zikiwemo mbili dhidi ya Yanga na Azam FC pale Sokoine.

Pili:
Msimu huu, timu zikikutana na Mbeya City, zinajua kuwa zinakwenda kupambana na nani na kuifunga ni zaidi ya ushindi. Hivyo makocha na wachezaji wanajiandaa vilivyo na hiyo inaonyesha ugumu wa kila mechi kwao.

Si kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa kuwa hakuna aliyejiandaa kupita kiasi dhidi yao.

 Tatu:
Hili linaweza likawaudhi, lakini nidhamu kwenye kikosi cha City imeshuka, tena hii ni hadharani kwa vitendo. Wamekuwa wakigombana au kuwazonga waamuzi bila ya woga, ujeuri wa wazi na huenda ni mafanikio yamewasahaulisha.

Achana na nje ya uwanja, kuna matukio ya wachezaji hao kuteremka kwenye basi lao, barabarani na kuwapiga madereva kisa wameziba njia. Wao si askari wa usalama barabarani, hauwezi kusikia Cristiano Ronaldo kazozana na dereva wa lori eti kisa amelizuia basi la Real Madrid lisipite.

Kiburi si maungwana, hakuna aliyefanikiwa kupitia kiburi, badala yake juhudi, malengo na kuepusha kuvimba kichwa. Jamani, matatizo yanamfanya mtu akue zaidi. Kyala awasajo.


MATOKEO:

      MECHI                                     UWANJA

1. Mbeya City       0-0       JKT       Sokoine

2. Mbeya City 1-0  Coastal       Sokoine

3. Ruvu             0-0   Mbeya          Mabatini

4. Mbeya City       0-1       Azam       Sokoine

5. Mbeya City       0-2       Mtibwa       Sokoine

6. Mgambo       2-1       Mbeya       Mkwakwani

7. Stand           1-0       Mbeya          Kambarage


MSIMAMO BARA:

       P       W       D       L       F       A       GD       PTS      
1. Mtibwa    7       4       3       0       10       3       7       15      
2. Yanga       7       4       1       2       9       5       4       13      
3. Azam        7       4       1       2       8       4       4       13      
4. Coastal     7       3       2       2       9       7       2       11      
5. Kagera     7       2       4       1       6       4       2       10      
6. JKT           7       3       1       3       7       7       0       10      
7. Simba        7       1       6       0       7       6       1       9      
8. Polisi          7       2       3       2       6       7       -1       9      
9. Mgambo    7       3       0       4       4       7       -3       9      
10. Stand       7       2       3       2       5       9       -4       9      
11.  Ruvu       7       2       1       4       4       7       -3       7      
12. Prisons    7       1       3       3       6       7       -1       6      
13. Ndanda    7       2       0       5       8       13       -5       6      
14. Mbeya       7       1       2       4       2       6       -4       5      
        
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment