MAWASILIANO

Phone. - +255 (717) 300 260 - +255 (787) 300 260

HABARI YA MUJINI

HABARI YA MUJINI
watu wa mpira


Na Ben Shija
SIMBA ndiyo hivyo imeanza Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Sports. Maana yake imefuta hofu kuu ya mashabiki wa timu hiyo.

Unakumbuka msimu uliopita? Simba ilipata sare sita katika mechi zake za kwanza na kuzua hofu kubwa. Huenda hilo limeondoka na sasa inaweza kuingia kwenye hesabu ya timu zinazowania ubingwa kama itaendeleza ushindi.
SIMBA DUME-TEMBONI imefanya mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe siku moja kabla ya mechi hiyo ya Simba ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, lengo kutaka kujua kama ameridhika na usajili huo na utaifikisha Simba ambako Wanasimba wanatarajia baada ya maumivu makali ya msimu uliopita.
“Nimeridhika, naweza kusema kwa asilimia tisini nimeridhika, lakini hapa sasa linafuata suala la kuangalia timu inacheza vipi na kama kuna upungufu tena, basi tunajua nini cha kufanya,” anasema Hans Poppe.
SALEHJEMBE: Kwa hali ilivyo, inaonekana Simba mmetumia fedha nyingi maana mmekuwa mkileta wachezaji wengi bomu!
NIANG

 Hans Poppe: Kweli kuna wachezaji walikuwa bomu, lakini si gharama ya Simba na kama ipo ni kidogo sana. Nimeona mmekuwa mkilaumu, lakini hamjui mambo yalivyo.
Kawaida mawakala ndiyo wamekuwa wakiwaleta wachezaji wao na gharama ya tiketi inakuwa yao.

SALEHJEMBE: Kama mchezaji mkimkubali, bado inakuwa ni gharama ya wakala na utaratibu uko vipi hadi wamlete mchezaji?
Hans Poppe: Kama mchezaji tumeona anafaa, basi gharama zote za safari zinakuwa juu yetu. Kama hatujamkubali, gharama ni za wakala.

Kuhusu utaratibu, hawa mawakala ni watu wanaouwinda msimu, wakijua dirisha liko wazi wanakutafuta, wengine nilikutana nao World Cup kwenye (Fainali za Kombe la Dunia), hivyo tukawa na mawasiliano.
 
OKWI
SALEHJEMBE: Mawakala kutoka Afrika Magharibi wanajulikana kwa utapeli, mliliangalia hilo?
Hans Poppe: Tuko makini sana kuliko mnavyofikiri, ndiyo maana hata wachezaji ambao mawakala hawakutaka wafanye majaribio mimi nilisisitiza lazima wafanye majaribio. Mfano yule bomu Papa Niang, wakala wake alilazimisha asifanye majaribio, nikakataa.
SALEHJEMBE: Vipi mlimuuza Okwi wakati ndiye alikuwa injini ya kikosi, hamuoni mlikurupuka na fedha yenyewe haikuwa ya kutisha?
Hans Poppe: Hakika haikuwa fedha nyingi sana, tumemuuza kwa dola 110,000 (Sh milioni 220,000). Awali wale jamaa walimtaka kwa dola 150,000 lakini tulikataa na hii inaonyesha hatukuwa tayari kumuuza.

Ilionekana Okwi anataka kwenda, aliamua kutumia kile kipengele cha kwenye mkataba ambacho anaweza kununua mkataba wake. Niseme kweli alituvuruga kwa kuwa hakikuwa kipindi mwafaka cha kumuuza na hatukutaka.

Ndiyo maana utaona, wale Al Markhiya, juzi hapa wamerudi wanamtaka tena Kazimoto kwa dola 150,000 lakini tumekataa, maana tutakuwa tunavuruga timu kila wakati.
 
MAVUGO
SALEHJEMBE: Unaridhika na safu yenu ya ushambuliaji ambayo inaonekana kumkosa Laudit Mavugo na imekuwa ni kama tatizo kwenu?

Hans Poppe: Kwa sasa ninaweza kusema ndiyo, tuna Mgosi (Hassan), Kiiza (Hamis) unajua ni wazuri kwa kufunga. Yupo Ajibu pale, tunaweza kwenda tukapambana na kufanya vizuri.

Kuhusu Mavugo kweli, tulikuwa ndiyo tumempa nafasi ya ushambuliaji, lakini Warundi ni watu wanaoishi bila utaratibu katika soka. Hadi leo hata ITC ya yule beki hawajatuma, hali kadhalika Wakongo nao hawajatuma ITC ya Lyanga, ni tatizo sana.
Ndiyo maana tukakimbilia kwa Kiiza, angalau ni mtu ambaye tunamjua na hatuwezi kuwa na hofu sana.
SALEHJEMBE: ITC hazijatumwa, nanyi mmeamua kulala hadi zitakapotumwa hata iwe mwakani?
Hans Poppe: Hapo sasa ndiyo TFF wanapaswa wafanye kazi yao, hayo ni mawasiliano ya shirikisho na shirikisho na hata ikishindikana wanaweza kutuombea kibali cha muda Fifa. Nashangaa wamekaa kimya tu, anayeshughulikia masuala ya uhamisho kwani hajaliona hilo?
SALEHJEMBE: Yule Msenegali mliyemsajili, mmeridhika au presha tu mkaona acha mfunike kombe?
Hans Poppe: Hapana, yule ni mchezaji kijana na anaonekana ana vitu vizuri. Anahitaji muda na benchi zima la ufundi limekubali na kumpitisha.

Utaona ana umbo zuri, mrefu ana futi 6.6 si mchezo. Atakuwa tatizo kwa makipa na baadaye lazima atasumbua sana. Mimi nina imani naye, pia atafanya vema hasa kama akiwa na malengo.
SALEHJEMBE: Kipa raia wa Ivory Coast alikuja Azam FC, wamemuacha ghafla kaja kwenu, mmemsajili na mkaachana na Ivo Mapunda! Hii ilikuwa katika mipango?
 Hans Poppe: Kweli hatukuwa na mpango naye, lakini usumbufu wa Ivo ndiyo ulichangia tuanze kuangalia njia mbadala. Alikuwa mtu tunayemuamini ndiyo maana tulimlipa hadi fedha za usajili mapema tu.

Shida ikawa ni yeye kuja kusajili, kila mara ana udhuru, sijui hivi sijui vile. Nyie hamjui mambo ya ndani, wachezaji wa Tanzania wana mambo yanaudhi sana.

Tukaona tusije tukaingia kwenye aibu ya kuingia msimu mpya bila kipa, tungechekesha. Huyu kipa kutoka Ivory Coast ni mzuri, mzoefu ingawa kapewa kazi ya kuhakikisha anakuwa fiti hasa.
 
HANS POPPE...
SALEHJEMBE: Ikitokea usajili wa Simba ukaonekana haukuwa mzuri, uko tayari kubeba lawama kama mwenyekiti wa kamati?
Hans Poppe: Lawama kivipi? Kamati ya usajili haipaswi kubeba lawama yoyote kama usajili utakuwa na walakini. Hamjui utaratibu unavyokuwa kabla ya mchezaji kusajiliwa.

Kuna njia nyingi lakini kamati ya ufundi ndiyo inayoleta majina, kamati ya usajili inafanyia kazi na baada ya hapo benchi la ufundi linahusika.
Sasa kwa nini uilaumu kamati ya usajili? Nafikiri ambao hawajui kuhusu hili, wanapaswa kulielewa namna hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment