Kama ulipitwa na kipindi cha Sports Bar cha jana kupitia Clouds TV bado hujakosa kitu, kwasababu kupitia shaffihdauda.co.tz unaweza kupata kila kitu kilichozungumzwa na Afisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara ambaye alikuwa mgeni katika kipindi hicho na alipata fursa ya kuzungumza na kutoa ufafanuzi juu ya mambo mawili makubwa ambayo kwa sasa ndiyo habari ya mjini kwenye klabu hiyo.
Jambo la kwanza ni kuhusu klabu hiyo kutakiwa na bilionea wa kitanzania Mohamed Dewji ‘MO’ na msimamo wa klabu hiyo hadi sasa lakini jambo la pili ni kuhusu klabu hiyo kumtimua aliyekuwa kocha wao mkuu Dylan Kerr baada ya kukiongoza kikosi chao kwa miezi kadha kwenye ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Manara amezungumza mengi lakini kuhusu suala la klabu ya Simba kutakiwa na MO Manara alitoa ufafanuzi kwa kusema viongozi wa Simba wanapenda klabu yao iendeshwe kisasa, lakini MO hakufuata taratibu zinazotakiwa katika kufikisha maombi yake ya kutaka kuiendesha Simba kama kampuni.
“Kiuhalisia viongozi wote wa Simba wangependa timu iendeshwe kisasa, atokee mtu, watu au taasisi waiendeshe timu katika mfumo wa kampuni, tulipata kusikia mwenzetu mmoja hapa ilizungumzwa sana mitandaoni na kwenye vyombo vya habari kwamba anataka kuichukua klabu ya Simba aiendeshe. Hakuna aliyekataa lakini ni lazima tuambiwe itaendeshwa kwa namna gani”, alisema Manara wakati akiwa kwenye mazungumzo ya kipindi cha Sports Bar ndani ya Clouds TV.
“Simba ni klabu ya umma ni lazima iende kwa taratibu. Bwana mkubwa yule angeleta document juu ya meza akawapa uelewa wajumbe wa kkamati ya utendaji wa kile anachotaka kukifanya waridhike wapeleke kwenye mkutano mkuu kungekuwa hakuna tatizo. Lakini yeye ametoa ultimatum kwa uongozi kwa muda wa siku tatu matokeo yake mambo yakija kuharibika utalaumiwa uongozi huu uliopo madarakani”.
“Ilikuwa lazima ifanyike process, juzi nilikuwa nazungumza na Rais wa klabu ameniambia amezungumza na MO, MO amekataa kwamba hakutoa ultimatum kwa uongozi wa Simba”.
Kwa upande mwingine Manara alitaja sababu za uongozi wa Simba kumtupia virago aliyekuwa kocha wao mkuu Dylan Kerr mara baada ya kutupwa nje ya Mapinduzi Cup. Manara amesema Kerr hakuwa na kikosi cha kwanza, hataki ushauri kutoka kwa makocha wenzake lakini kubwa ni kwamba, wana Msimbazi wanataka kuona timu yao inashinda.
“Sitaki kuzungumzia makocha wa nyuma, lakini Kerr labda kiongozi mwendawazimu ndiyo angekubali kuendelea kukaa naye. Miezi sita sasa Simba haina ‘first eleven’, halafu Kerr hana anayemshauri siyo uongozi, hata makosha wenzie”, alisema Manara wakati alipouzwa sababu za kumtimua Kerr.
“Mimi nilikuwepo Zanzibar, alipokuja huyu kocha wetu mpya Mayanja nikampokea nikampleka kumtambulisha kwa Kerr. Neno la kwanza aliloniambia ni kwamba, huyu tayari nimeshapata habari zake, huyu ni ‘mafia’ sana kaja hapa kunishughilikia mimi akamtaja kocha mmoja wa Uganda kwamba ndiyo amemwambia kuhusu habari za Mayanja”.
“Kerr ndiye aliyemuondoa kocha wetu wa viungo, kamuondoa Matola ambaye amekaa na makocha wote zaidi ya nane hakuna hata mmoja aliyewahi kulalamika kuhusu Matola. Lakini tukasema huyu ndiyo chief coach tumuheshimu. Kabla ya kumleta Mayanja tulitaka kumleta Basena lakini Kerr akamkataa kwasababu baadhi ya watu walimwambia basena hata wezananae”.
“Lakini kubwa kuliko yote, sisi tunataka matokeo lakini hadi leo Simba bado haina kikosi cha kwanza. Mimi mwenye ukiniambia nikutajie kikosi cha kwanza cha Simba sikijui, hakuna timu hiyo duniani”.
Manara akamaliza kwa kusema, uongozi wa klabu ya Simba utaanza ujenzi wa uwanja wao wa Bunju kuanzia juma lijalo wakianza na sehemu ya kuchezea ‘pitch’ halafu itafuatiwa na majukwaa.
0 comments:
Post a Comment