Samatta akiwa ubalozi wa Ubelgiji |
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta leo amepatiwa viza ya kwenda Ubelgiji kujiunga na klabu ya KRC Genk.
Taarifa ya Ubalozi wa Ubelgiji nchini imesema kwamba, Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika alitembelea ofisi hizo na kupatiwa viza.
“Mchezaji Bora wa Afrika 2015/16, Mbwana Ally Samatta ametembelea Ubalozi wa Ubelgiji kwa ajili ya kuchukua viza ya kwenda kujiunga na KRC Genki nchini Ubelgiji,”imesema taarifa ya Ubalozi ya Ubelgiji.
Ubalozi wa Ubelgiji umemsifu Samatta kama mchezaji mwenye malengo haswa, kipaji na anayejitambua kama mchezaji wa Tanzania, hivyo wanamtakia kila la heri katika maisha yake mapya Ubelgiji.
Ingawa bado klabu yake, TP Mazembe haijatangaza rasmi, lakini taarifa zinasema mwishoni mwa mwaka jana, Rais wa klabu hiyo ya DRC, Moise Katumbi alifikia makubaliano na klabu hiyo ya Ubelgiji juu ya biashara ya mchezaji huyo.
Na kwa Samatta kwa kupatiwa viza ya kwenda Ubelgiji, maana yake anahitimisha miaka yake minne ya kuishi Lubumbashi, yalipo makao makuu ya TPM, klabu bingwa ya Afrika mara ya tano.
Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, anaondoka Mazembe baada ya kuichezea mechi 103 na kuifungia mabao 60.
Kijana huyo wa umri wa miaka 24, anaondoka Mazembe akiiachia taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.
0 comments:
Post a Comment