Mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Mrundi, Amissi Tambwe, ameutaka uongozi wa klabu hiyo
kumpa barua ya kuondoka klabuni hapo kama umemchoka na siyo kumsingizia mambo
ya ajabu ambayo hajafanya na wala hatarajii kuyafanya.
Tambwe
ambaye alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Vital’O ya Burundi na
kufanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mabao
19, hivi sasa hana amani tena katika kikosi cha timu hiyo.
Hali
hiyo inatokana na hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Simba kumtaja kuwa anaihujumu
timu hiyo akishirikiana na baadhi ya wachezaji wenzake.
Tambwe amesema kuwa kama wamemchoka ni bora wakampatia barua ya kuachana na
klabu hiyo na siyo kumchafulia jina.
Alisema
amechoshwa na tuhuma hizo ambazo zinamfanya atumie muda mwingi kuzitafakari
japokuwa hazina ukweli wowote na kushindwa kufikiria mambo ya msingi
yatakayomwezesha kufanya vizuri katika mechi zijazo za timu hiyo.
“Sasa
ndiyo naamini yale niliyokuwa naambiwa na wachezaji wenzangu wa Burundi waliowahi
kuzitumikia timu za Tanzania kuwa hata ufanye mema mangapi ipo siku
utadharaulika na utaonekana mtu usiyefaa kabisa.
“Mema
yote na kujitolea kwangu uwanjani nilikofanya msimu uliopita ili kuhakikisha
tunafanya vizuri leo hii naonekana sifai, eti naihujumu Simba kwa sababu tu
sifungi, hakika naumia sana.
“Katika
soka kuna mambo mengi ambayo yanaweza kumkuta mchezaji, kutofunga kwangu siyo
kwamba nafanya makusudi nimekuwa nikijitahidi sana kutafuta nafasi lakini mambo
yanakuwa magumu kwa sababu timu nyingi zimejiandaa vizuri na wachezaji wengi
msimu huu wapo makini sana na mimi ndiyo maana hali hiyo imetokea hivyo sipaswi
kulaumiwa.
“Kama
wanaona nafanya makusudi basi wanipe barua ya kuachana na mimi na siyo
wasinichafulie jina langu kwa kunisingizia mambo ambayo sijafanya,” alisema
Tambwe ambaye msimu huu amefunga bao moja katika mechi nne alizocheza.
0 comments:
Post a Comment