Ayoub Nyembo ‘Masai’ akiikagua barua ya uchumba na posa kabla ya kumkabidhi mshenga.
WAZO LILIVYOIBUKA
Mtu wa karibu na Masai alilipenyezea gazeti hili habari kuwa, baada ya habari za Wema kummwaga mpenzi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuandikwa magazetini hivi karibuni, fasta Masai aliiona fursa ‘u-single’ kwa Wema, akatangaza nia ya kumposa kwani alikuwa akimzimia muda mrefu.
“Masai ametumia fursa, hakutaka kuchelewa maana wazo alikuwa nalo kitambo lakini alishindwa kufanya hivyo kwa kumhofia Diamond,” alisema mtu huyo.
Ayoub Nyembo ‘Masai’ akiikabidhi posa kwa shujaa wake yaani mshenga.
AKUTANISHWA NA IJUMAA WIKIENDA
Baada ya mtu huyo wa karibu na Masai kupata mawasiliano ya Ijumaa Wikienda kisha alikutanishwa nalo maeneo ya Mwenge jijini Dar akiwa tayari ‘amejikoki’, mkononi akiwa na barua ya uchumba sambamba na bahasha yenye shilingi elfu hamsini kama posa.
Ijumaa Wikienda: Unataka kumuoa Wema kweli au unazingua?
Masai: Nipo ‘serious’ ndiyo maana unaona nimekuja kwako nikiwa kamili na mshenga wangu nipeleke kwa mama Wema.
...Kisha Ayoub Nyembo ‘Masai’ akitoa muongozo kwa mshenga wange katika kuiwasilisha posa hiyo.
SAFARI KWA MAMA WEMA
Huku mwanahabari wetu akigonga picha za kumwaga kwa kila hatua, alimwelekeza Masai huyo ambaye pia ni msanii wa Bongo Fleva nyumbani kwa mama Wema, Mariam Sepetu ‘Mkwe’ ambapo waliambatana na mshenga wake lakini walipokaribia, Masai alikaa sehemu na kumtuma mshenga azame ndani.
Mshenga akimalizia safari kuelekea kwa mama mkwe.
NDANI KWA MZAA CHEMA
Mshenga alipozama ndani, alikutana na mfanyakazi wa ndani (house girl) ambaye alipokea barua hiyo ya uchumba na kumpelekea moja kwa moja mama Wema.
Mshenga akiwasili kijasiri getini kwa wahusika.
BARUA YASOMWA
Baada ya kutua mikononi mwa mama Wema, aliisoma barua ya uchumba kisha akamuomba mshenga kuingia ndani huku akiwa na furaha hususan pale alipogundua kuwa mkwewe mtarajiwa (Masai) ni mtu wa Kigoma.
MAZUNGUMZO YA FURAHA
“Kwa hiyo Wema wangu anatakiwa aolewe Kigoma akale migebuka eeh?,” mama alimuuliza mshenga.
Mshenga akilonga jambo na binti (house girl) kufikisha ujumbe kwa mkwe.
Bila hiyana mshenga akajibu: “Ndiyo mama, Masai anaishi Kigoma ila ana nyumba zake Dar, huwa anakuja mara kwa mara kwenye biashara zake na pia ana mji Singida katika Kijiji cha Ikungi na ni mfugaji mzuri, ng’ombe anao wa kutosha.”
Mshenga akisepa baada ya kumaliza majukumu mazito.
POINTI YA MSINGI
Shangwe zaidi iliongezeka kwa mama Wema baada ya kusikia Masai huyo ana mji Singida tena kwenye kijiji ambacho yeye anatokea akatoa masharti kuwa afuate taratibu za Kitanzania kwa kumtaka Masai azungumze na Wema kisha ampigie simu ndiyo apokee barua kwa amani.Hii ni barua ya uchumba iliyoandikwa na mmasai, Ayoub Nyembo.
HUYU HAPA MAMA WEMA
“Hili ni jambo la kheri jamani, nimekuelewa lakini uchukue barua hii sambamba na posa urudi kwanza ukamwambie huyo mkwe mtarajiwa azungumze na Wema wakikubaliana, Wema yeye ndiye aniambie siku ya ninyi kuja kutoa posa ili na mimi nijiandae,” alisema mama Wema.
-GPL