Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Bobby Williamson amewataka Simba kuongeza nguvu ya kumnasa mshambuliaji nyota wa Gor Mahia, Danny Sserunkuma.
Akizungumza na BEN SHIJA kutoka Nairobi, Kenya, Williamson aliyewahi kuinoa Gor Mahia na kuipa ubingwa amesema Sserunguma raia wa Uganda ana uwezo mkubwa katika safu ya ushambuliaji.
“Simba hawatajuta kumsajili Sserunkuma, ana kasi, ana uwezo mkubwa wa kutoa pasi za mabao, kuichosha safu ya ulinzi ya timu pinzani.
“Anafunga mabao yakiwemo yale ya muhimu, yaani anafunga katika kipindi ambacho mnaamini haiwezekani.
“Kama sijakosea msimu uliopita alifunga mabao kumi na tatu, lakini alitoa pasi nyingi na alikuwa msaada kwa timu,” alisema.
Tayari Simba iko katika hatua nzuri ya mazungumzo na Sserunkuma ambaye anataka kubadili ‘hali ya hewa’ baada ya kukaa Kenya zaidi ya miaka mitatu.
Mganda huyo aliwahi kuwaniwa na Yanga kabla ya baadaye kubadili uamuzi na kumtwaa Emmanuel Okwi.
Taarifa zinaeleza Simba imetakiwa kutoa dau la dola 15,000 (Sh milioni 24) ili kumpata Sserunkuma ambaye mara ya mwisho kucheza Tanzania ilikuwa ni siku Gor Mahia iliposhindiliwa mabao 3-0 na Simba katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
0 comments:
Post a Comment