THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Website : www.ikulu.go.tz               

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
     STATE HOUSE,
             1 BARACK OBAMA ROAD,   
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taratibu za Tiba za Rais zakamilika

Taratibu za matibabu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, zimekamilika leo, Jumatatu, Novemba 24, 2014.

Taratibu hizo za matibabu za Mheshimiwa Rais Kikwete zimekamilika kiasi cha saa 12 asubuhi ya leo wakati madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mjini Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, walipomfanyia hatua ya mwisho ya tiba.

Hata hivyo, Rais Kikwete ataendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.

Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 29, 2014.

Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.

Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.