MASHABIKI na wanachama wa Simba wamejitokeza kwa wingi katika mechi maalum ya Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi.
Umati wa mashabiki waliojitokeza wakati Simba ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya SC Villa ya Uganda, umewashangaza watu wengi sana.
Asilimia kubwa ya wapenda soka walikuwa wakiamini mashabiki wa Simba wamekata tamaa kutokana na mwenendo wa timu yao kwa miaka mitatu sasa.
Simba imekuwa ikijipoza kwa kuifunga Yanga pekee au kubeba lile Kombe la Nani Mtani Jembe baada ya ushindi dhidi ya watani wao Yanga.
Ukiachana na hapo, Simba si ile ya zamani ambayo ilikuwa kama imekosa ubingwa, basi iko katika nafasi ya pili.
Simba imekuwa si ile ambayo kama ikikosa ubingwa lakini ikapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, basi habari yake utaiona. Inajulikana Afrika nzima hata nchini Misri ambao ni vigogo wa soka la Afrika, ukiwaeleza Simba wanaijua ni timu machachari na isiyotabirika kutokea Tanzania.
Wakati uongozi wa Rais Evans Aveva unaingia madarakani, uliikuta Simba tayari imeingia katika kundi la waliochoka. Yaani haina ubingwa mkononi wala haipati nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Kama nilivyoeleza, sifa kubwa ya Simba ilikuwa ni kuifunga Yanga, jambo ambalo mashabiki wa Simba wamelibakiza kama sehemu yao ya furaha linapozungumziwa suala la mafanikio.
Lakini katika uhalisia, kuifunga Yanga pekee wakati Simba haina nafasi ya kubeba ubingwa wa Tanzania Bara ni kichekesho. Au kuishinda Yanga wakati Simba haiwezi kushiriki michuano ya kimataifa hata ile ya Afrika Mashariki na Kati ni dharau!
Simba ni kubwa, Simba ina historia ya juu katika soka la hapa nchini hata kama itakuwa haifanani na timu nyingine kubwa kama Zamalek ya Misri au Al Hilal ya Sudan.
Watu waliojitokeza juzi kwenye Uwanja wa Taifa ndiyo jibu sahihi kwamba klabu hiyo ni kubwa. Tena waliojitokeza, kuna rundo walibaki nyumbani huenda kwa kukosa nafasi au kukata tamaa.
Kwa msimu uliopita, uongozi wa Aveva unaweza ukawa una nafasi ya kujieleza kwamba ulikuwa ukijaribu kubadili mambo kadhaa ili kurejea katika ramani sahihi ya kupambana na kurejesha heshima ya Simba.
Lakini kwa msimu huu, hakika hakutakuwa na visingizio vyovyote wala haitakuwa rahisi kutengeneza mbeleko ya kuwabeba wanachama na mashabiki wanaoipenda klabu yao.
Waliokwenda pale uwanjani wamefungua mfuko wa deni kwa uongozi wa Simba na wanapaswa wajue wanachama wale wanachotaka ni furaha kutoka kwa klabu hiyo hasa kwa kuiona timu yao ikishinda na kuondoka katika dimbwi la masimango kwamba wao ni “Wa hapahapa”.
Maandalizi yaliyofanyika yameonekana, yanaweza kupewa maksi za maandalizi bora hata kama haitakuwa ni asilimia mia. Lakini mwisho kitakachoangaliwa ni matokeo yakoje.
Simba haiwezi kuwa ya kuonewa kila msimu, iko chini ya Yanga na Azam FC, wakati mwingine inakwenda hadi chini ya Mbeya City.
Sasa ni wakati wa kurejesha heshima kwa uongozi wa Aveva kufanya kazi kwa juhudi na mipango sahihi kuhakikisha Simba waliyopewa inaanza kutoa majibu na si hadithi pekee kwamba wanabadili kikosi.
Kati ya mashabiki wavumilivu duniani, wale wa Simba ni miongoni mwao. Huenda huu ukawa ni msimu wa mwisho kuonyesha uvumilivu huo kama mambo yataendelea kuwa vile.
Wakati uongozi ukipambana, wanachama na mashabiki nao wanatakiwa kuwa pamoja, kushirikiana na uongozi kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanatimia ili Simba irejee katika hadhi yake ya kuwa moja ya timu bora barani Afrika.
0 comments:
Post a Comment