Ushindi wa jana wa Azam ilioupata kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi uliwaengua Simba katika nafasi ya pili ambayo kwa sasa inakaliwa na Azam FC yenye pointi 58 huku Simba ikishuka kwa nafasi moja hadi nafasi ya tatu kwa pointi zake 57 wakati huo wakiwa wanalingana idadi ya michezo waliyocheza wapinzani wake katika mbio za ubingwa pamoja na ile iliyosalia ili ligi kumalizika.
Yanga, Azam na Simba zote zimecheza michezo 25 hadi sasa huku mechi tano pekee ndizo zimebaki kuamua nani atainyanyua ndoo ya VPL msimu huu na wale ambao watateremka kwenda ligi daraja la kwanza kujiuliza walikosea wapi wakati wako VPL.
Simba imeishia kuliona kwa macho tu kombe la VPL kwa miaka mitatu mfululizo iliyopita wakati kombe hilo likitua Chamazi na mitaa ya Twiga na Jangwani.
Msimu huu Simba walikaa kwenye njia nzuri mara baada ya kikosi chao kuwa chini ya Jackson Mayanja aliyekabidhiwa timu hiyo siku chache baada ya kutimuliwa aliyekuwa kocha mkuu Dylan Kerr kutokana na timu kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya Mapinduzi Cup January 2016 wakiwa ndiyo mabingwa watetezi wa taji hilo.
Mayanja aliajiriwa Simba kama kocha msaidizi lakini kwa bahati mbaya hakusimama kwenye benchi la ufundi hata mara moja kwenye michuano ya Mapinduzi kwasababu siku aliyotua Zanzibar ndiyo timu yake iliyaaga mashindano.
Mayanja akarejea Dar na kufanikiwa kukiongoza kikosi cha Simba kushinda michezo 6 mfululizo ya VPL, Simba iliifunga Stand United kwa bao 2-1 February 13 ukiwa ndiyo ushindi wao wa sita mfululizo kwenye ligi wakiwa chini ya Mayanja. Ikumbukwe ushindi huo uliifanya Simba kukwea hadi kileleni mwa ligi kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2013-14.
Hapo wachezaji wa Simba, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wakawa na imani timu yao itafanya vizuri na huenda ikachukua taji la ligi kuu msimu huu ambalo wamelikosa kwa muda sasa.
Baadaye mambo yakaanza kubadilika taratibu na hadi kufikia sasa, Simba iko nafasi ya tatu huku ikiwa inalinga na wapinzani wake kwa idadi ya mechi walizocheza na zile zilizosalia ili ligi kufikia tamati.
Mchezo wa Simba vs Azam utakaopigwa Jumapili ya wiki hii ndiyo utaamua hatma ya Simba katika kuwania ubingwa wa VPL msimu huu, Simba inahitaji ushindi tu ili kuendelea kuziweka hai ndoto zake za kuibuka bingwa wa ligi msimu huu. Matokeo tofauti na hayo yatazidi kufifisha matumaini yao hususan kama watapoteza pambano hilo.
Simba kama itashinda game hiyo itakuwa na pointi 60 wakati huo Yanga tarari itakuwa imeshacheza na Toto Africans kwahiyo kama Yanga watakuwa walishinda watakuwa na pointi 65, sare ya Yanga itawafanya Simba wawe nyuma yao kwa pointi tatu na endapo Yanga watafungwa basi watairuhusu Simba iwe nyuma yao kwa tofauti ya pointi mbili pekee.
Azam wakiruhusu kufungwa na Simba itawalazimu kuwa nyuma ya Simba kwa pointi mbili zaidi na kuzidi kuua matumaini ya kutwaa taji la VPL msimu huu baada ya kulikosa msimu uliopita na kuambulia nafasi ya pili.
Ili Simba iweke hai matumaini ya kuchukua ubingwa wa VPL msimu wa 2015-16 ni lazima ishinde mbele ya Azam kwa nammna yeyote ile, swali linaloibuka hapa ni kwamba, Azam atakubali kufanywa ngazi na Simba kuelekea mwisho wa ligi au Azam ndiyo itazima matumaini ya Simba kutwaa ubingwa wa VPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu?
0 comments:
Post a Comment