Na Ben Shija
HAKUNA anayeweza kukataa kwamba Watanzania wamekuwa wakililia sana kuona Tanzania inakuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi yetu.
Wadau wanaamini hilo ni sehemu ya kujifunza mambo mengi na kuwasaidia wachezaji kujua mambo mengine mapya ambayo wakirejea nayo nyumbani, basi yataanzisha mbio mpya ya mabadiliko ya soka hapa nchini.
Ingekuwa inawezekana wachezaji wengi wa Tanzania wakaenda kukipiga Ulaya hiyo ingekuwa bora zaidi, lakini si vibaya hata kama wataanzia nchi za jirani kabla ya kupiga hatua zaidi kwenda huko.
Tumeona kwa Mbwana Samatta ambaye amepata mafanikio na TP Mazembe ya DR Congo, sasa anapiga hatua kwenda mbele. Ninaamini Watanzania wana matarajio makubwa na Thomas Ulimwengu pia.
Wako Watanzania wengine ambao pia tunaamini wana nafasi ya kwenda nje ambako tunaamini kunaweza kutusaidia kwa wachezaji wetu kujifunza mambo mengi ikiwemo nidhamu, upendo wa kimichezo, malengo na mengine mengi.
Nimeamua kuandika makala haya baada ya kushangazwa na rafu mbili tu za mkongwe Henry Joseph ambaye mimi nimemuona akicheza akiwa kinda hadi sasa anajulikana kama mkongwe.
HENRY J WAKATI AKIWA SIMBA, HAPA ILIKUWA MECHI DHIDI YA MTIBWA |
Nakumbuka alikuwa akicheza Simba wakati huo anatokea Shule ya Sekondari ya Makongo. Alikuwa akionekana ni mchezaji ambaye atafanya vema baadaye. Kocha wake Mbrazili wakati huo alisisitiza hilo, tena akisema Tanzania itaweza kufanikiwa kama itawajali na kuwapenda wachezaji makinda.
Kocha huyo aliwahi kusisitiza, kwamba amekuwa akizungumza na wachezaji wakongwe kuwajali wachezaji makinda ili waweze nao kupiga hatua. Labda kabla ya kueleza ninachotaka kusema, nimkumbushe hilo Henry, kwamba lazima awajali wachezaji makinda kama ambavyo yeye wakongwe walivyomjali wakati ule.
Ingawa ni rafiki yangu, lakini niende mbele zaidi na kumueleza kwamba katika mechi ya kwanza, ilikuwa Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga, Kombe la Mapinduzi, nilishuhudia Henry akitolewa nje kwa kadi nyekundu, dakika chache baada ya kuwa ameingia uwanjani.
HANRY J WAKATI AKIKIPIGA NORWAY |
Alilambwa kadi nyekundu, baada ya kadi ya pili ya njano, safari hii akiwa amemparamia kiungo Salum Telela wa Yanga. Hakika ilikuwa ni faulo ya uchezaji wa mchangani au uswahilini kwetu ambayo isingeonekana ya ajabu, lakini ingelalamikiwa.
Faulo hiyo ilionyesha kabisa, Henry aliruka kwa makusudi kwenda kumkanyaka Telela na wala hakuwa na nia ya kumzuia au kuchukua mpira. Ilinishangaza, lakini nikaona huenda ni ubinadamu, kila mmoja anakosea.
Lakini ndani ya wiki moja, Henry amerudia jambo kama lile lililonishangaza. Safari hii katika mechi dhidi ya Simba Uwanja wa Taifa, juzi. Henry alilambwa kadi nyekundu kwa kumrukia teke la Kung Fu kiungo kinda wa Simba, Ibrahim Ajib, kabla ya hapo alimkanyaga kwa makusudi na kumuumiza Peter Mwalyanzi.
Ajib alitolewa nje akiangua kilio, sijui ni kwa nini. Huenda alikuwa shabiki wa Henry wakati akicheza Simba na yeye bado akiwa shule anasoma. Sasa anahuzunishwa na namna alivyogeuka ‘mnyama’ kwake na kumrukia mgongoni kama mtu aliyetamani kusimamisha ndoto zake za kuendelea kucheza soka!
Usisahau, kabla ya hapo, Henry alimrukia tena beki kinda wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye alilala chini akigugumia maumivu. Bado ilionekana haikuwa rafu ya bahati mbaya au mtu aliyekosea kitu, badala yake lilikuwa ni pigo la shabaha.
Mapigo matatu ya Henry ndani ya wiki moja tena yote kwa wachezaji makinda yananishangaza. Ninashindwa kujua kusudio na wala siwezi kukubali jambo la bahati mbaya badala yake nabaki najiuliza, “hivi Henry hapendi vijana, au Henry ana chuki na vijana!”
Henry alianzia kinda kwenda kuwa mkongwe, sasa wamemkosea nini vijana, sehemu ambayo hata yeye alipita? Lakini nikawa najiuliza, nini faida ya kucheza soka Ulaya? Maana Henry alicheza nchini Norway kati ya wachezaji wa Tanzania wanaotokea Ulaya kuja kuichezea timu ya taifa.
Ana mambo mawili makubwa tayari ambayo yangemfanya uchezaji wake uyatoe kama ushahidi. Kwanza ni ukongwe, lazima angekuwa mfano na mfano mzuri kwake ni Shabani Nditi ambaye ni nahodha wake, ninaamini unanielewa vizuri.
Pili, kacheza Ulaya; sasa ilimsaidia nini kama anachoonyesha hajali kuumiza wenzake, hajali kuwakatisha vijana ambao ndiyo wanaanza kupigania kutimiza ndoto zao. Hajali kutolewa nje kwa kadi nyekundu na kuisababisha Mtibwa kucheza pungufu. Ukongwe wake na kucheza kwake Ulaya, faida yake nini sasa!
0 comments:
Post a Comment