Ushindi wa sita mfululizo kwenye ligi unazidi kutengeneza mazingira na ishara nzuri kwa kocha Mganda Jackson Mayanja ambaye tayari ameshinda mechi saba hadi sasa tangu atangazwe kupewa nafasi ya kocha msaidizi siku chache kabla ya kupigwa chini kwa aliyekuwa kocha mkuu wa ‘mnyama’ Dylan Kerr kutokana na kufanya vibaya kwa timu yake kwenye mashindano ya Mapinduzi, Zanzibar.
Mayanja anasema siri ya kupata matokeo mazuri ni wachezaji kushika maelekezo na mbinu anazowapatia huku akisisitiza nidhamu ya wachezaji ni kitu kingine kinachosaidia timu yake kufanya vizuri.
Ushirikiano anaoupata kwa wachezaji kwa kufuata kila anachowaelekeza mazoezini lakini pia ushirikiano kutoka kwa viongozi na mashabiki ambao wanasafiri na timu kuishangilia kila inapokwenda.
Baada ya mechi dhidi ya Stand United, simbadumetemboni.co.tz ilitaka kujua sasa mpango mzima wa kocha kuelekea mchezo ujao dhidi ya Yanga. Mayanja ambaye amekuwa maarufu tangu atue msimbazi kuliko muda wote aliofundisha timu za Kagera Sugar pamoja na Coastal Union, akatia ngumu kuweka wazi ni dozi gani ataibuka nayo kwenye game yake dhidi ya watoto wa Jangwani.
“Kwasasa siwezi kuzungumza chochote kuhusu mechi ya Yanga, nataka kujua kwanza wachezaji wangu wangapi wameumia kwasababu kuna wachezaji tuliwatoa kutokana na kuumia kwa mfano Hassan Kessy”, amesema Mayanja ambaye miaka ya nyuma aliwahi kutamba kama mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda.
“Mambo yote kuhusu Yanga nitazungumza Jumatatu kwasababu hao Yanga wenyewe hawapo nchini, nawasubiri kwanza waje nyumbani”.
Simba na Yanga zitakutana February 20 kwenye mchezo ambao Yanga watakuwa wenyeji wakiwa wanachagizwa na ushindi wao wa ugenini kwenye mchezo wa klabu bingwa Afrika wakati Simba wanamorali ya ushindi tangu kutua kwa Mayanja kwenye mtaa wa Msimbazi.
0 comments:
Post a Comment