Shirikisho la soka nchini Nigeria (Nigeria Football Federation) liliwahi kuzisimamisha timu nne ambazo zilihusika kwenye scandal ya upangaji matokeo baada ya timu mbili za ligi ya chini ambazo zilikuwa zinahitaji kupanda daraja huku zikihitaji ushindi wa tofauti ya magoli na zikashinda mechi zao kwa bao 79-0 na 67-0. Hiyo ilikuwa ni miaka mitatu iliyopita (July 10, 2013).
Kwenye mechi ambazo zilichezwa muda mmoja, Plateu United Feeders iliripotiwa kufunga magoli 72 kipindi cha pili na kufanikiwa kuifunga Akurba FC 79-0. Police Machine wakaifunga Babayaro FC magoli 61 ndani ya dakika 45 kwenye ushindi wao wa magoli 67-0.
Shirikisho la soka Nigeria iliita tukio hilo kuwa ni ‘mchezo wa akili’ na wa aibu na kuongeza kuwa wachezaji, maofisa waliosimamia mechi hiyo na mratibu wa mashindano inabidi wachunguzwe kwa tuhuma za upangaji matokeo.
Mkurugenzi wa mashindano alisema, mtu yeyote ambaye atagundulika kuhusika na mchezo huo mchafu atashughulikiwa kikamilifu.
Jana lilitokea tukio ambalo linafanana na hilo kwenye soka la Tanzania baada ya vilabu viwili vya ligi daraja la kwanza vinavyowania kupanda daraja kucheza ligi kuu msimu ujao kupata matokeo ambayo yaliwastusha wengi.
Geita Gold FC na Polisi Tabora zote zikiwa kundi C ligi daraja la kwanza, zilikuwa zimelingana kwa kwa pointi, zote zilikuwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 14 huku timu hizo zikiwa zimefungana pia kwa idadi ya magoli ya kufunga ambapo zote zilikuwa na magoli 20 lakini zilitofautiana kwa magoli ya kufungwa. Geita Gold ilikuwa imefungwa magoli 6 wakati Polisi Tabora wao walikuwa wamefungwa goli 5.
Mchezo wa mwisho ndiyo ulikuwa unaamua nani atapanda kucheza ligi kuu msimu ujao, kutokanana kulitambua hilo kila timu ilitambua kuna uwezekano mkubwa wa bingwa kuamuliwa kwa tofauti ya magoli.
Geita ikashinda mechi yake kwa magoli 8-0 dhidi ya JKT Kanembwa wakati Polisi Tabora wao wakailaza JKT Oljoro kwa bao 7-0.
Matokeo hayo yakazifanya timu hizo kufanana kwa kila kitu pointi hadi tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Baada ya matokeo ya jana, TFF ilitangaza haitotangaza mshindi wa kundi C hadi hapo vyombo husika vitakapopitia kwa makini taarifa za michezo hiyo miwili na kujiridhisha kabla ya kutangaza mshindi.
Hatua hiyo imekuja baada ya aina ya matokeo na nafasi zilizokuwepo timu hizo kutoa harufu ya upangwaji wa matokeo wa michezo hiyo.
0 comments:
Post a Comment