Na Baraka Mbolembole
Mapema mwezi Januari, 2015 nilipata kuandika makala kuhusu uwezo wa kiuchezaji wa mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars,) Musa Hassan Mgosi. Akiwa katika msimu wake wa pili katika timu ya Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro, Mgosi alikuwa tayari amejijengea tabia ya kuzifunga Yanga SC na Simba SC ambayo awali alipata kuichezea kwa mafanikio kati ya mwaka 2005 hadi 2011.
Kiwango chake cha juu katika michuano ya Mapinduzi Cup, 2015, Zanzibar kiliisaidia mno Mtibwa kufika fainali ya michuano hiyo ambayo walipoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti mbele ya Simba. Nakumbuka niliandika makala ya kuwashawishi Simba kumrejesha kikosini mwao mshambulizi huyo ambaye alishinda mataji ya ligi kuu msimu wa 2007 na 2009/10 akiwa na ‘Wekundu hao wa Msimbazi.’
Kuna vitu ambavyo Simba kama timu ndani ya uwanja wanakosa tangu walipofanya makosa ya kuwaacha wachezaji wengi wazoefu waliokuwa na ubora mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2012/13.
Msimu ambao wachezaji kama aliyekuwa nahodha, golikipa, Juma Kaseja, walinzi Shomari Kapombe, Amir Maftah, Juma Said Nyosso, Haruna Moshi ‘Boban,’ Mrisho Ngassa, Ramadhani Chombo ‘Redondo,’ Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto, Salum Machaku ambao waliachana na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa msimu kwa sababu mbalimbali.
Simba wanakosa wachezaji wazoefu wanaoifahamu kihistoria ya klabu na kimahitaji, wazoefu ambao ubora wao kiuchezaji ungeweza kuwasaidia wachezaji vijana waliopewa nafasi kujifunza na kupata ukomavu kwa msaada wa wale wenye uzoefu.
Wakati naandika makala yale, Mganda, Emmanuel Okwi ndiye alikuwa nguzo pekee ya timu ndani ya uwanja lakini hata mshambulizi huyo hakutosha kiuzoefu ndiyo maana nilihitaji kuona Mgosi anarejeshwa Simba baada ya kuonesha kiwango kizuri kiuchezaji akiwa na Mtibwa katika misimu ya 2013/14 na 2014/15.
Nilifarijika kuona Simba wamemrejesha mchezaji huyo wakati wa usajili katikati ya mwaka uliopita. Tena, wakampa na unahodha wa timu (majukumu ambayo kwa msimu mmoja nyuma yalikuwa kwa kijana, mlinzi wa kati, Hassan Isihaka.)
Kabla ya kuanza msimu timu ilifanya maandalizi ya muda mrefu (zaidi ya wiki 6) huku ikiwa na makocha watatu, Muingereza, Dylan Kerr aliyekuwa kocha mkuu, Mzawa, Suleimani Matola, kocha wa makipa raia wa Kenya na yule mtaalam wa mazoezi ya viungo kutoka Serbia.
Jopo hilo la benchi la ufundi na urejeo wa wachezaji wanaoifahamu timu kama Mgosi na kiungo, Kazimoto kulichukuliwa kama sababu kubwa ya kwanza ambayo ingeweza walau kurudisha makali yaliyotoweka katika timu hiyo kuanzia katikati ya mwaka 2012. Mimi sikuwa na imani bado, na nilitilia shaka zaidi kwa kuwa kuna watu katika uongozi wa juu ndani ya klabu si waelewa wa mambo ya soka.
Tazama, Mgosi yule ambaye alipaswa kucheza kwa nguvu uwanjani na kufunga magoli ili timu ipate matokeo amekuwa ‘kocha mchezaji!’ Majukumu ambayo analazimika kuyakubali kwa maana uongozi umechukulia kirahisi tu kucheza zaidi ya game 20 wakiwa bila kocha mkuu.
Nitaendelea kuwaita ‘mafionso-genge la wahuni’ baadhi ya watawala wa timu hiyo kwa maana katika mazingira ya ushindani huwezi kupata mafanikio katika timu yako ikiwa na kocha mmoja tu. Tena kocha huyo alichukuliwa kama msaidizi wa kocha mkuu ambaye alipaswa kuchukua nafasi ya Kerr aliyetimuliwa mapema mwezi Januari mwaka huu kwa sababu ya matokeo.
Mgosi chini ya Kerr alipata nafasi ya kuwa anaanza sambamba na Mganda, Hamis Kiiza ambaye naye amesajiliwa msimu huu, lakini baada ya kiwango kizuri cha ufungaji kutoka kwa kijana, Ibrahim Ajib aliyekuwa akitokea benchi, taratibu Mgosi akaanza kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza kwa sababu kama mshambuliaji hufungi goli katika michezo mfululizo, ni sawa na kushindwa kutimiza majukumu yako.
Hadi sasa, Mgosi hajapata kuifungia Simba goli lolote katika game za mashindano tangu aliposajiliwa katikati ya mwaka jana. Kwa mshambuliaji ni sawa na ‘kushindwa’ kwa kiasi kikubwa. Viongozi wa Simba wanakila sababu ya kulaumiwa. Unawezaje kuendesha timu kwa kocha mmoja eti kwa kigezo cha kutegemea uzoefu wa baadhi ya wachezaji?
Hivi huyu Mgosi anakidhi matakwa ya kiushauri kwa kaimu kocha mkuu, Jackson Mayanja? Nimesikia kiongozi mmoja wa juu wa timu hiyo majuzi akisema kwamba wataleta kocha mpya. Mimi nataka niwaulize nyie viongozi, wanachama, ama mashabiki wa Simba kama ni haki timu yenu kucheza mechi zaidi ya 20 za mashindano muhimu bila kuwa na kocha mkuu.
Mayanja alichukuliwa kuziba nafasi ya Matola lakini baada ya kushinda ‘mechi 6’ mfululizo kila mtu akawa kimya kuhoji ujio wa kocha mbadala wa Kerr na yule kocha wa makipa raia wa Kenya.
‘Mgosi alisajiliwa kucheza mpira au kuwa mshauri wa kocha na wachezaji vijana? Mmebugi sana Simba SC. Kumbukeni huu ni msimu wa nne mnatoka ‘kapa’ VPL! Mgosi alisajiliwa kuwa kocha/mshauri au mchezaji?
0 comments:
Post a Comment