IDDI SALIM... |
Kocha wa makipa wa Simba, Abdul Salim, raia wa Kenya, amefunguka kuwa endapo msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ukianza bila ya kuwa na kipa mkongwe Ivo Mapunda, ni pigo kubwa kwa timu hiyo.
Uongozi wa Simba kupitia kwa ofisa habari wake, Haji Manara, umetangaza kuachana na Ivo lakini Salim ameliambia gazeti hili kuwa mkongwe huyo anahitajika kikosini.
Ikumbukwe kuwa, awali kocha huyo wa makipa mara tu alipoanza kazi Simba, alitamka kuwa anahitaji aletewe kipa mzoefu atakayekuja kusaidiana na Ivo katika kuipa mataji Simba ambapo alipendekeza asajiliwe kipa wa Gor Mahia, Boniface Oluochi lakini akatua Muivory Coast, Vincent Angban.
Salim alisema, yeye kama kocha hawezi kuzungumzia kiundani masuala ya kimkataba yanayomhusu Ivo lakini anachoweza kueleza ni kwamba kama wakimpoteza kipa huyo, basi watakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha makipa waliopo wanafanya kile Wanasimba wanachokihitaji.
Aliongeza kuwa, Ivo ni mmoja kati ya makipa wazoefu, hivyo uwepo wake kwenye timu unaongeza ari, lakini kikubwa viongozi wao ndiyo wana maamuzi ya mwisho kwani wao ndiyo waajiri wakuu na ndiyo wenye mamlaka ya kuamua chochote.
“Makipa nilionao kwa sasa si wabaya, wanajitahidi kuonyesha uwezo wao ambao unanipa matumaini, hatupo na Ivo kwenye mazoezi kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi na nimesikia kwamba bado hajaongezewa mkataba wa kuitumikia Simba.
“Suala la kimkataba siwezi kulizungumzia kutokana na kwamba mimi siyo muajiri wake, lakini kikubwa ni kwamba kama tukimpoteza basi tutakuwa na pengo katika timu,” alisema Salim ambaye kabla ya kutua Simba aliwahi kuzifundisha timu za Gor Mahia, FC Leopards pamoja na timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.
0 comments:
Post a Comment