Mshambuliaji wa kimataifa wa Azam FC kutoka nchini Burundi Didier Kavumbagu, amesema kuwa yupo tayari kuondoka kwenye klabu hiyo kama ataendelea kusugua benchi kwenye klabu hiyo.
“Kwanza namshukuru mwenyezi Mungu kwa kuweza kunipa nafasi, pili nashukuru kwa wale wote ambao wameweza kunipa nafasi kama mwalimu pamoja na benchi zima la ufundi”, amesema Kavumbagu ambaye alifunga goli la kwanza wakati Azam ikishinda goli 4-2 dhidi ya JKT Ruvu.
“Nimeweza kuonesha kile ambacho nakijua, sijui kama ni mwalimu anapenda kuniweka benchi lakini mimi najiamini kwamba najua mpira na naweza kufanya kitu cha ziada cha kusaidia timu”.
“Ushindani upo lakini mimi siwezi kusema kwamba kuna ushindani mkubwa sana, kikubwa ni mwalimu aniamini na kunipa nafasi ya kucheza. Kwasababu nikipata nafasi ya kucheza nafunga”.
“Mimi sioni kama kuna ushindani mkubwa zaidi kwasababu wachezaji wengi ni wale ambao walikuwepo tangu mwaka jana, hakuna kitu ambacho kimebadilika kwa upande wa Azam. Wachezaji ni walewale na, ni mwalimu kuniamini tu na kunipa nafasi”.
“Leo amenipa nafasi nimeonesha kama ninakitu cha kufanya kuisaidia timu lakini kama hanipi nafasi siwezi kumlazimisha kunipanga. Karibu mechi saba sijacheza lakini nimerudi leo nimeonesha uwezo nilionao, leo ni mechi ya nane lakini nimevumilia tu”.
“Ni kawaida kwenye mpira anaweza kuja mwalimu mpya akakuweka nje, tunaona hata Ulaya lakini mimi navumilia. Kama itawezekana nitabadilisha timu, kama ikiwezekana hata katika dirisha dogo naweza nikabadili timu, siwezi nikavumilia kukaa nje mimi sijazoea kukaa nje”.
“Timu zipo nyingi mimi najua kazi yangu, nilikuja Tanzania kucheza mpira sikuja kukaa nje, nikikaa nje sawa lakini dirisha dogo naweza nikabadili timu au nisibadili yote ni kawaida”.
Kavumbagu amekuwa akianzia benchi kwa muda mrefu kwenye kikosi cha Azam FC huku John Bocco, Kipre Tchetche na Alan Wanga wakipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho kuliko yeye.
0 comments:
Post a Comment