MAWASILIANO

Phone. - +255 (717) 300 260 - +255 (787) 300 260

HABARI YA MUJINI

HABARI YA MUJINI
watu wa mpira

KUTOKA OUAGADOUGOU, 2007 HADI N’DJAMENA, 2016, ERASTO NYONI AMEANZA MECHI ZOTE 40 STARS, ANAFUNDISHA…


Erasto Nyoni mchezaji wa Azam FC na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'
Erasto Nyoni-Mchezaji wa Azam FC na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
Na Ben Shija
Unajifunza nini kutoka kwa kiungo-mlinzi wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na klabu ya Azam FC? Mechi yake ya 40 Stars (dhidi ya Chad)  ilizima wasiwasi wote wa Watanzania kuhusu uwezo wa mchezaji huyo ambaye aliitwa tena na kocha Charles Boniface Mkwassa baada ya kuwa nje ya timu tangu katikati ya mwaka uliopita wakati Stars ‘ilipoboronga’ katika michuano ya mataifa ya Kusini mwa Afrika ( COSAFA Cup) nchi Afrika Kusini.
KLABU 3 TU TANGU 2005
Erasto alisajiliwa AFC Arusha na kucheza kwa mara ya kwanza ligi kuu Tanzania Bara. Mkufunzi, Madaraka Bendera alimsajili Erasto akiwa kinda U17 akitokea kikosi cha academy ya Rolling Stone pia ya Arusha.
Baada ya msimu mbaya uliopelekea kushuka daraja kwa AFC, Erasto alijiunga na klabu ya Vital’O ya Burundi mapema mwaka 2006 na alicheza ligi kuu ya Burundi hadi katikati ya mwaka 2008 aliporejea nyumbani na kuichagua Azam FC badala ya klabu kubwa za Yanga SC na Simba SC ambazo pia zilikuwa zikimuhitaji.
Ameendelea kuwa mchezaji muhimu katika timu ya Azam FC hadi sasa licha ya kukutana na changamoto za mara kwa mara za majeraha na kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza, Erasto ananivutia kwa ukimya wake na kutopenda kulalamika hovyo katika vyombo vya habari.
Kuna wakati alipata majeraha makubwa ya goti kiasi cha kumuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, lakini aliporejea alijibidiisha na kuwa fiti tena.
Kwa wachezaji wa mwanzo waliosajiliwa Azam FC mara baada ya timu hiyo kupanda VPL katikati ya mwaka 2008, Erasto ndiye pekee aliyejibidiisha na kufanya vizuri kiasi cha kudumu kwenye timu hiyo kwa misimu yake yote ya ushiriki wa VPL.
Nahodha, John Bocco, na vijana wengine wachezaji wa nafasi ya kiungo, Salum Abubakary na Himid Mao ndiyo wachezaji wengine pekee ambao wanaungana na Nyoni kama wachezaji wa muda mrefu zaidi.
Tofauti yao ni kwamba, wakati, Bocco, Himid na Salum wao wameichezea Azam FC tu katika maisha yao yote wakitokea timu ya pili, Erasto ni kati ya sajili za kwanza ghali klabuni hapo kumuhusisha wacheza wazawa.
MARCIO MAXIMO ALIMTOA KUSIKOJULIKA NA KUWA NYOTA WA NCHI
Wakati wa utawala wa mkufunzi, Mbrazil, Marcio Maximo kama kocha wa Taifa Stars (2006-2010) alijaribu pia kutazama maendeleo ya wachezaji wa Kitanzania waliokuwa wakicheza nje ya nchi. Nafikiri, Erasto ndiye mchezaji aliyefanikiwa zaidi kati ya wale ambao Maximo aliwaita kwa nyakati tofauti wakitokea nje ya nchi.
Maximo alisisitiza zaidi kuhusu wachezaji kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, na aliwapa kipaumbele zaidi wachezaji ambao walikuwa watiifu. Nidhamu ya Erasto iko juu sana, ni msikivu na mtu anayependa kujituma katika mazoezi.
Maximo alipenda kumtumia Erasto kama mchezaji wa akiba. Alipoitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya Taifa alikuwa kama mlinzi wa kati, chaguo la nne nyuma ya Salum Sued ‘Kussi’, Victor Costa ‘Nyumba’ na Hamisi Yusuph ‘Waziri wa Ulinzi’.
Mechi yake ya kwanza Stars ilikuwa ni ile dhidi ya Burkina Faso (2007) ugenini katika kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za CAN 2008 nchini Ghana. Stars ikiwa na wachezaji wengi wenye majeraha katika beki za pembeni, Maximo akampanga Nyoni katika beki 3 isivyotarajiwa na wengi.
Ni nafasi hiyo iliyompa umaarufu mkubwa Nyoni kwa wapenzi wa kandanda nchini. Wakati huo (2007) wachezaji mastaa wa Stars walikuwa ni wale waliokuwa wakichezea klabu kubwa za Simba na Yanga. Lakini baada ya kufunga goli pekee la uwezo binafsi ambalo liliipa Stars nafasi ya kuwa sambamba na waliokuwa vinara wa kundi, Senegal kwa kufungana alama.
Erasto, akawa staa mkubwa na watu wakaanza kufuatilia kujua anachofanya katika klabu yake ya wakati huo Vital’O. Kila mchezaji alipata si chini ya milioni 7 zilizochangwa na wadau wa mpira nchini wakiongozwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushindi ulikuwa mtamu sana na mechi ile ndiyo ilifungua njia ya mafanikio kwa Erasto katika soka lake nchini.
Hadi sasa ameichezea timu ya taifa game 40. Mechi 9 za michuano ya kufuzu kwa CAN, Mechi  3 za michuano ya kuwania kufuzu CHAN (Kumbuka Erasto alipata majeraha makubwa siku moja kabla ya Stars kwenda katika michuano ya CHAN nchini Ivory Coasta 2009-Michuano ya kwanza kabisa ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani).
Ameiwakilisha Stars mara 5 katika michuano ya kufuzu kwa fainali za kombe la dunia, mechi nyingine 3 za michuano ya COSAFA, mechi 15 za kimataifa kirafiki na mechi nyingine 5  za michuano ya CECAFA Challenge Cup akiwa na timu ya Tanzania bara (Kilimanjaro Stars).
Kitu kingine cha kupendeza ni kwamba mchezaji huyo aliyezaliwa Mei 7, 1988 huko Songea ameanza katika kikosi cha kwanza katika game zote hizo 40 alizoiwakilisha nchi.
Ni mshindi wa VPL taji ambalo alishinda msimu wa 2013/14, pia mara mbili ameshinda taji la ligi kuu ya Burundi. Novemba 2012 mchezaji huyo ‘kiraka’ alituhumiwa kupokea rushwa ili Azam ifungwe.
Lakini baada ya uchunguzi yakinifu uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Kushwa nchini-TAKUKURU mchezaji na wenzake, Deogratius Munish ‘Dida’ na Aggrey Morris wakarejeshwa kundini baada ya kuwa nje ya timu kupisha uchunguzi.
Aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa (2012-14) Kim Poulsen aliendelea kumuita kikosini na kumtumia Erasto. Huyu ni mchezaji wa mfano pia kwa vijana wanaochipukia.


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment