Nahodha wa zamani wa Barcelona Xavi Hernandez, amemuelezea Lionel Messi kama mchezaji bora kuliko Cristiano Ronaldo, na pia mwenye akili nyingi zaidi ya nyota huyo wa Madrid ambaye ni mpinzani wake mkubwa kwa sasa ulimwenguni.
Messi na Ronaldo wamekuwa ni wachezaji wanaocheza kwenye kiwango cha juu kwa muda mrefu sasa, wakichuana vikali kwenye tuzo ya Ballon d’Or kwa miaka mitano mfululizo, huku Messi akishinda mara tatu ndani ya kipindi hicho na Ronaldo mara mbili.
Ronaldo kwa mara nyingine tena, yuko katika kinyanyiro cha kuwania ufungaji bora msimu huu, mpaka sasa akiwa ameshapachika mabao 28 La Liga, na kumwacha Messi mwenye magoli 22 licha ya Messi kuwa na uwiano mzuri wa ufungaji kwa dakika.
Alipoulizwa tofauti ya wawili hao, Xavi, ambaye kwa sasa anacheza nchini Qatar, alisema: “Ronaldo ni mfungaji, na Messi ni mfungaji pia; hata hivyo, Messi ni mchezaji mzuri kucheza kitimu zaidi ya Ronaldo.
“Nadhani Messi ni mchezaji bora kabisa ulimwenguni kwa sasa. Kwenye soka, kuna vitu viwili muhimu: kuwa fiti na kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri (intelligence). Ronaldo yuko fiti sana tu lakini Messi ana vitu vyote hivyo, utimamu na akili pia, sasa kwa vigezo hivyo Messi ni bora.”
0 comments:
Post a Comment