SIMBA SC wamehitimisha mechi zao tano za kirafiki kisiwani Unguja kwa kushinda mabao 3-2 dhidi ya washika magendo wa KMKM uwanja wa Amaan jioni ya leo.
Ushindi wa wekundu hao wa Msimbazi Dar es Salaam leo, umeifanya timu hiyo inayofundishwa na kocha Muingereza, Dylan Kerr inayojiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutopoteza mchezo wowote na pia kutokutoka sare.
Hata hivyo, mapema ilionekana pengine hadithi katika mchezo wa leo ingekuwa kinyume, kwani KMKM timu zilikwenda mapumziko KMKM ikiongoza 2-1.
Mussa Hassan Mgosi wa Simba SC (kushoto) akitafuta maarifa ya kuwatoka wachezaji wa KMKM leo |
KMKM inayonolewa na Ali Bushiri, kipa wa zamani wa Small Simba, Malindi na Zanzibar Heroes, ilianza kucheka na nyavu dakika ya 20 kwa bao la Mateo Simon kabla mchezaji huyo huyo kupachika tena mpira kimiani dakika ya 25.
Dakika nne kabla mapumziko, Mganda Hamisi Kiiza akaifungia Simba SC kufanya KMKM iwe mbele 2-1 wakati mwamuzi akipuliza firimbi ya kukamilisha kipindi cha kwanza.
Ibrahim Ajib aliinusuru Simba kwa kufunga mabao mawili dakika ya 71 na 75, na kuifanya iondoke na ushindi wa asilimia 100 katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na kundi lote la 'Friends of Simba'.
Kwa matokeo hayo, Simba inayoondoka kesho kurejea Dar es Salaam, imeshinda mechi zote tano za kirafiki ilizocheza ikiwa kambini hapa Zanzbar.
Awali iliifunga kombaini ya Zanzibar 2-1, ikaizamisha Black Sailors 4-0, baadae ikaichapa Polisi 2-0, Jang'ombe Boys 3-0 kabla ya leo kuinyuka KMKM 3-2.
0 comments:
Post a Comment