LICHA ya timu yake ya KCB kukubali kichapo cha mbwa mwizi cha mabao 6-1 kutoka kwa mabingwa watetezi na vinara wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, straika Paul Kiongera, ameendeleza moto wake wa kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
KCB ambao waliduwazwa kwa kichapo hicho wakiwa uwanja wao wa nyumbani, walijifariji kwa bao hilo moja ambalo liliwekwa wavuni na Kiongera aliyepo kwa mkopo kutoka Klabu ya Simba.
Simba walimsajili Kiongera msimu uliopita kutoka katika klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kenya, lakini alijikuta akicheza mchezo mmoja wa ufunguzi dhidi ya Coastal Union na kupata majeraha baada ya kugongana na aliyekuwa kipa wa Wagosi hao wa Kaya, Shaban Kado.
Kiongera aliumia vibaya goti na kupelekwa India ambako alipata matibabu na baada ya kupona Simba walimtoa kwa mkopo wa miezi sita kwenda KCB ili kurejesha kiwango chake.
Baada ya hapo, Simba walimrejesha jijini Dar es Salaam ili kucheza msimu huu lakini vipimo vikaonyesha bado hajapona vizuri na kuendelea kumwacha kwa mkopo KCB ambayo inafarijika kuwa naye kutokana na uwezo alionao wa kutupia mabao.
Hata hivyo, licha ya Simba kudai Kiongera hajapona, lakini kwa sasa ndiye lulu kwa KCB, kwani amekuwa akiisaidia mara kwa mara kutokana na uwezo wake wa kucheka na nyavu.
Katika msimamo wa Ligi Kuu nchini humo Gor Mahia ambao ndio mabingwa watetezi wapo kileleni wakiwa na pointi 49 katika michezo 19 waliokwisha kucheza mpaka sasa huku KCB wakiwa nafasi ya 13 katika michezo 22 waliyocheza na Kiongera akiwa na mabao tisa.
0 comments:
Post a Comment