Na Ben Shija
Mashabiki wengi wa Timu ya Simba hawana furaha kwa sasa.
Hawawezi kuwa na furaha kwa sababu timu yao wanayoipenda kwa dhati ya mioyo yao
imeshindwa kabisa kuwapa raha wanayoihitaji kwa muda mrefu sasa.
Kwa miaka mitatu mfululizo timu ya Simba imeshindwa kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) yaani tangu ilipoutwaa ubingwa huo katika
msimu wa 2011/2012 haijawahi kufanya hivyo tena.
Kwa mashabiki na wanazi wa klabu hiyo kamwe hawawezi
kuridhika na suala hilo asilani, ni lazima walalamike na kwa kiasi kikubwa
wengi wao wameonekana kuwa babaikoni kwa sasa.
Pengine ujio wa kasi wa klabu ya Azam FC umekuwa sababu ya
haya yanayotukia leo kunako klabu ya Simba, kwani kabla yake ilikuwa ni suala
la kawaida mno kwa ubingwa wa Ligi Kuu kuwa chini ya vilabu pinzani ‘Simba na
Yanga’.
Kama ndivyo sidhani kama kuna suala la kulalamika zaidi ya
viongozi wa klabu husika kuhakikisha kuwa wanajipanga kinaganaga kwa lengo la
kuendana na kasi ya ushindani wa Ligi husika.
Mashabiki wengi wa Simba wana ukame. Wanaitaka timu yao
ifute makosa ya muda mrefu ili iweze kuwapa raha kama ilivyokuwa zamani. Hakuna
namna nyingine ya kuweza kufuta makosa hayo zaidi ya kufanya usajili wenye
tija.
Kitu pekee ambacho kwayo kimekuwa kikiwapa ahueni mashabiki
hao wa Msimbazi ni matokeo mazuri ambayo wamekuwa wakiyapata mbele ya Yanga.
Pengine kwa kiasi fulani matokeo hayo yalipunguza hasira za mashabiki hao.
Lakini pamoja na ushindi wa mara kwa mara dhidi ya mtani
wake, bado mashabiki wa timu hiyo wanaitaka timu yao kwenda mbali zaidi wakiitaka
iweze kuchukua ubingwa na si kuifunga Yanga pekee.
Kitakwimu za soka la Tanzania ni wazi kuwa Timu ya Yanga
inaongoza kwa kuchukua mara nyingi zaidi taji la Ligi kuu (mara 25) huku Simba
SC ikifuatia baada ya kufanya hivyo mara 18.
Hata hivyo, timu ya Simba SC ndiyo timu pekee katika soka la
bongo yenye historia ya kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Kimataifa
kuliko klabu nyingine zote za ndani ya Tanzania.
Pengine rekodi zifuatazo zinaweza zikawapa hasira zaidi
mashabiki wa ‘Mnyama’ na hata kuwataka Viongozi wao kuhakikisha kuwa wanafanya
kila linalowezekana ili timu yao hiyo iwe bingwa wa VPL 2015/2016.
Ubingwa wa Kombe la Mapinduzi
Mapema mwaka huu (2015) Simba SC ilifanikiwa kuutwaa ubingwa
wa kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na hata kujikuta ikiweka rekodi adhimu
zaidi ya kulitwaa taji hilo mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote kutoka bara na
visiwani.
Simba imetwaa taji hilo mara tatu, lakini pamoja na kufanya
hivyo bado haijaweza kukata kiu ya mashabiki wake kuhusu kuuota ubingwa wa VPL
na hata kuwafanya mashabiki wao kujikuta wakiwasurutisha Viongozi wao kufanya
usajili wenye tija na siyo usajili wa ‘bora liende’.
Ubingwa Kombe la Kagame
Licha ya Yanga kujivunia rekodi ya kutwaa taji la Kagame nje
ya Dar es Salaam, Simba ndiyo vinara wa kulitwaa taji hilo nchini. Simba
imewahi kulitwaa taji hilo la Kagame mara sita na kuwa timu ya Bara yenye
historia ya kulitwaa zaidi kombe hilo kuliko timu nyingine yoyote.
Mbali na kuwa timu ya Bara iliyotwaa taji hilo mara nyingi,
Simba ndiyo timu inayoongoza kwa kutwaa Kombe la Kagame kwenye historia ya
michuano hiyo na kuzipiku timu zote za ukanda huo.
Rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la
shirikisho (CAF)
Wekundu wa Msimbazi ndiyo timu pekee ya Tanzania
iliyofanikiwa kucheza fainali za Kombe la Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika yaani
CAF. Ilikuwa mwaka 1993 wakati huo likijulikana kama Kombe la Caf.
Simba ilicheza fainali hiyo na Stella Abidjan ya Ivory Coast
na kutoka sare katika mchezo wa awali kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2- 0
katika marudiano jijini Dar es Salaam.
Licha ya Simba kupoteza mchezo huo ambapo wachezaji wake
waliahidiwa zawadi za magari kama wangeshinda, inasalia kuwa timu pekee kutoka
Tanzania Bara iliyofanikiwa kucheza hatua hiyo ya fainali hizo.
Nusu fainali klabu Bingwa Afrika
Historia ya klabu ya Simba inavutia! Ndivyo unavyoweza
kusema kwa lugha rahisi baada ya timu hiyo kufanikiwa kucheza nusu fainali ya
Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974.
Hata hivyo iliondolewa katika hatua hiyo ya nusu fainali na
klabu ya Mehala El Kubra ya Misri na kuzima ndoto za kucheza fainali ya
michuano hiyo mikubwa zaidi katika bara
la Afrika.
Rekodi hiyo ya Simba bado haijavunjwa mpaka leo hii ni timu
yoyote ya Tanzania, japo mwenendo wake kwa sasa unaonekana kuwaghafilisha
wanazi wengi wa timu hiyo kwa sasa.
Historia
ya kuiondosha Mashindanoni timu ya Misri
Mbali na rekodi tajwa hapo juu ambazo huenda zikazidi
kuchagiza machungu kwa mashabiki wa timu hiyo. Simba SC bado inajivunia rekodi
ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufanikiwa kuiondosha timu ya Misri
katika michuano ya Afrika.
Wanaume hawa walifanya hivyo mwaka 2003 baada ya kuifunga
Zamalek ya Misri ambayo ilikuwa inatetea ubingwa huo.
Pengine ninaweza nikawa nimewauzi mashabiki na wafuasi wengi
wa klabu ya Simba kwa maelezo hayo machache kuhusu klabu ya Simba. Lakini siku
zote ukweli huwa haujifichi.
Ni kweli rekodi na takwimu hizi tamu zinaifanya Simba ibaki
kuwa na historia nzuri na ya kuvutia kimataifa lakini kwa sasa haina jipya
kutokana na mwenendo wake usiotia matumaini.
Nitoe wito kwa viongozi husika kuhakikisha kuwa wanafanya
usajili wenye tija zaidi kwa lengo la kukiboresha kikosi chao na hata kuweza
kuirudisha heshima ya timu hiyo, heshima ambayo kwa sasa imeonekana kupungua.
Kwa nijuavyo mimi, hakuna linaloshindikana chini ya Jua. “Ni
kweli imebaki historia! Ngoja tuusubiri msimu mpya wa Ligi huenda ikaja
kivingine”.
0 comments:
Post a Comment