TULLY (KULIA) AKIZUNGUMZA NA KOCHA MKUU WA ORLANDO PIRATES WAKATI SIMBA ILIPOKUWA IMEWEKA KAMBI NCHINI AFRIKA KUSINI. |
MOJA ya mafunzo niliyopata ni kuhusiana na suala la kuripoti mechi moja kwa moja wakati ikiendelea. Si kwa kuzungumza, badala yake ni kwa kuandika.
Mafunzo hayo niliyopata kutoka kwa wataalamu wa Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), yalisaidia kubadilisha mwelekeo na hisia, au mazoea ya kile ambacho nilijifunza awali na haraka nikang’amua kuwa dunia inakwenda kwa kasi kubwa, ndiyo maana natamani kujifunza zaidi.
Moja ya malalamiko makubwa yaliyowahi kutolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakati wa uongozi wa Leodegar Tenga ni kwamba wasemaji wamekuwa hawazungumzi mambo sahihi wanayotakiwa kuzungumza.
Kwamba utakuta msemaji wa timu anazungumza kama mwalimu wa timu. Si ajabu ukamsikia anasema watacheza 4-4-2 kwa kuwa wameamua kuweka washambuliaji mbele, na blah blah au vinginevyo.
Pia unaweza kumsikia msemaji akitumia muda mwingi akizungumzia mwalimu au mwamuzi wa mechi fulani akionyesha kutovutiwa na kilichotokea katika mchezo. Uongozi wa Tenga, ukasema haikuwa sahihi.
Inawezekana itakuwa vigumu kuamini kwa kuwa tunahitaji kujifunza zaidi, ndiyo kabla sijapata mafunzo ya AFP, kuna mambo niliyachukulia tofauti hadi nilipojifunza na kugundua nilikuwa nyuma ya wakati.
Huenda ni wakati mwingine wa wasemaji kuendelea kujifunza ingawa nimekuwa nikishangazwa na kufurahishwa na mmoja wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully.
Nafahamiana na Tully takribani miaka kumi iliyopita, wakati akiwa mchezaji, alipoondoka nchini na baadaye kurejea. Tumekutana mara kadhaa na kuzungumza mambo ya kawaida au ya mpira.
Kinachonivutia ni namna ambavyo amekuwa akizungumza kwenye vyombo vya habari, anavyojibu na hasa mpangilio wa majibu kutokana na swali na kamwe hauwezi kusikia kaingia idara si yake.
Tully amekuwa mwepesi kung’amua wapi muuliza maswali anampeleka, kipi sahihi katika wakati mwafaka na upi mpaka wake wa kujibu maswali. Yeye si msemaji wa Simba.
Unakumbuka wakati fulani uongozi wa Simba ulisema umewasimamisha viongozi kuzungumza, lakini ilionekana hakuwa Tully kwa kuwa kabla hakuwa amemshambulia au kusema maneno yasiyofaa kwa mchezaji.
Inawezekana kabisa Tully akawa hajasomea masuala ya uzungumzaji, yaani si mwandishi wa habari. Lakini utulivu wake, wepesi wa kugundua mipango yake mwisho ni wapi inamsaidia kuweza kuzungumza sahihi na kutoa ufafanuzi sahihi kulingana na swali.
Kila mmoja anaweza kuwa na mtazamo wake, nimetumia zaidi ya wiki tatu kumfuatilia Tully nikitaka kujua anakopita kwa majibu kwa kila swali analoulizwa. Waingereza wanasema ‘perfect’. Yaani anapita katika mistari sahihi na hakuna maswali.
Huenda siku moja akakosea kwa kuwa naye ni binadamu lakini ukweli anachokifanya sasa kinaweza kuwa mfano kwa wasemaji wengine ambao sisemi wanafanya vibaya ila wanaweza kujinoa kupitia kwake baadhi ya mambo kwa nia ya kujiimarisha zaidi kuwa wapite njia ipi iliyo sahihi.
Tully kamwe hajawahi kuchanganywa na maswali ya jamaa hapo chini (Maulid Kitenge) wala mwenzake. Hajawahi kujibu kwa kushambulia chombo cha habari, mchezaji au mtu fulani, badala yake anakwenda kwenye hoja.
Si wasemaji wa timu tu wanaweza kujifunza. Hata watu wazima, viongozi wa Yanga, Simba pia nao wanaweza kujifunza kupitia Tully kwamba anazungumza kwa kujibu hoja kutokana na anachokielewa, si kutunga hadithi na swali linajibiwa kwa lawama au kushambulia tu. Ili mradi mahojiano yanakamilishwa na lawama au mashambulizi.
Tully hawezi kujua kila kitu kama mimi na wewe, lakini ameonyesha kwamba bado kuzungumza kwa kufuata weledi kunaweza kufanikiwa kwa umakini tu wa mtu. Hivyo msikilizeni, ubora wake uwe fundisho, machache anayokosea, pia yatumike kama mafunzo.
0 comments:
Post a Comment