MAWASILIANO

Phone. - +255 (717) 300 260 - +255 (787) 300 260

HABARI YA MUJINI

HABARI YA MUJINI
watu wa mpira

EXCLUSIVE: WANATAKA KUCHEZA MICHUANO YA KIMATAIFA, ILI IWEJE? WAKATI UMESHINDWA KUAJIRI HATA WATU WATANO- MICHAEL WAMBURA


wambura1.jpg
Ayoub Elias
MAPEMA asubuhi ya Jumanne nilimtafuta katibu mkuu wa zamani wa Chama cha soka Tanzania ‘FAT’ (sasa Shirikisho la Soka Tanzania-TFF,) na klabu ya Simba SC Ndugu Michael Wambura ambaye alikuwa ni mmoja wa wanachama wa klabu hiyo waliojitokeza kugombea nafasi ya urais klabuni hapo Juni 2014-kabla ya baadae kuondolewa ‘kimagumashi’ na aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi, wakili Dr. Damas Ndumbaro.
Nimekuwa wazi kila mara kuwa nimekuwa mfuasi wa sera za Wambura ambaye amekuwa na mtazamo wa kuifanya Simba kama taasisi ikue kiuchumia na kimpira kwa maana ya timu kufanya vizuri katika michuano ya ndani na nje ya nchi.
Miaka miwili ya utawala wa Evans Aveva ambaye alikuwa mshindani wa Wambura katika nafasi ya urais katika uchaguzi uliopita, nimekuwa na ‘shauku’ ya kutaka kujua kama si kufahamu mtazamo wa Wambura kama mwanachama wa klabu kuhusu mwenendo wa klabu yao ambayo imenakwenda kumaliza msimu wa nne pasipo taji la ligi kuu mwishoni mwa wiki hii.
Kumbuka Wambura anazungumza kama mwanachama wa kawaida tu.
www.simbadume.co.tz: Heshima yako kiongozi (baada ya kuitikia.) Unaonaje mwenendo wa klabu yenu hivi sasa ndani ya uwanja na nje ya uwanja ambako mambo yanaonekana kutokwenda vizuri. Klabu inawezaje kuepuka hali hii ya sasa ambayo si nzuri?
Michael Wambura: Unajua kuna sababu nyingi, kuna mambo mengi katika matokeo haya ya Simba na kinachoendelea kiujumla wake. Nianze na sababu za ndani ya uwanja. Kwanza sidhani kama wachezaji wa Simba ni wabaya kiasi hicho. Ni wazuri tu japokuwa inawezekana wasiwe na ubora mkubwa sana. Kuna ‘mpasuko’.
Kwa maana  kuna tofauti nyingi miongoni mwa viongozi wenyewe, kuna tofauti miongoni mwa wanachama, na kuna tofauti ndani ya timu kwa maana ya wachezaji. Na hii ni sbbabu mojawapo inayosababisha Simba kuwa katika hali hii ya sasa. Lakini pia kuna tofauti nyingine, kuna wanachama wamegawanyika katika makundi.
Kuna makundi ambayo yana sapoti uongozi na kuna makundi ambayo hayatoi sapoti, nadhani umenielewa. Na yale makundi yanakwenda mpaka ndani zaidi kiasi kwamba, hawa wengine wanajiona ni sehemu ya klabu, na wengine wanajiona ndiyo wamiliki wa klabu. Sasa katika mazingira hayo kunakosekana umoja, hivyo hamuwezi kufanya vizuri.
Pia kuna wachezaji ambao wanalipwa vizuri zaidi ya wengine, na wengine wanafanywa waonekane bora kuliko wengi. Hilo nalo ni tatizo. Unajua timu ya mpira wa miguu kwa sisi Tanzania ambako bado hatujapiga hatua katika mpira wa kulipwa, wachezaji wanatakiwa kuwa karibu sana na viongozi kwa maana ya kutatua matatizo.
Kitu ambacho nakiona kama hakifanyiki ndiyo maana tunasikia, mishahara inachelewa, timu imetelekezwa, timu imesafiri kwa daladala. Hii inamaanisha viongozi hawako karibu na wachezaji, hilo nalo ni tatizo lingine kubwa sana lililopo kwa jinsi navyoona mimi.
Lakini lingine kubwa ni udhaifu katika benchi la ufundi. Nafikiri kwa misimu hii mitatu Simba imekuwa chini ya makocha zaidi ya watatu. Sasa mnapokuwa hamuwezi kukaa na mwalimu na kudumu naye hata kwa miaka miwili lazima mtafeli. Mara zote makocha wanaingia wakati timu imeshasajiliwa.
Sasa wachezaji huwa wanasajiliwa na nani.? Ni udhaifu mkubwa. Kawaida ya mwalimu wa mpira wa miguu anasajili wachezaji kulingana na mifumo anayotegemea kufundisha, sasa kila anapokuja mwalimu anakuta timu imeshasajiliwa, atafanya nini.
Tofauti naangalia kwa wenzetu, mfano, Yanga, wamekuwa na kocha wao kwa kipindi cha pili sasa au cha tatu sasa na anajua mchezaji mzuri yupi, mapungufu yake wapi pamoja na kwamba unaweza kusema si bora lakini ‘angalau’ unaona kuna kitu wenzetu wanakifanya. Hata na mfumo wenyewe wa kiutawala wanao.
Kwamba, hapa kuna klabu, hapa kuna utawala, na hapa kuna watu wanafanya maamuzi. Lakini kwa sisi (Simba ) naona kuna tofauti katikati.
Kingine ambacho ni kikubwa kuliko vyote ni kwamba, Simba wana uchumi mbovu pamoja na kupata pesa za kina Samatta (Mbwana) na Okwi ( Emmanuel) lakini bado Simba hawana uwezo wa kifedha.
Ngoja nikwambie kitu kimoja, suluhisho la klabu si kuiuza klabu. Umenielewa vizuri? Ni lazima muingie mikataba na wadhamini wanaoeleweka. Kuinadi bidhaa-Simba inapaswa kunadiwa, kwa hiyo ina maana kwamba idara yenyewe ya masoko ya klabu ya Simba bado haijafanya kazi.
Bado wanategemea mapato ya milangoni. Hamuwezi kuendelea hivi, lazima kuwe na fedha zinajulikana zipo mahali fulani nje, zinakuja na kutumika katika taratibu zenu nzuri. Mna sajili wachezaji wazuri, mnakuwa na kocha mzuri, mnasafiri vizuri, mna walipa wachezaji mishahara vizuri.
Huwezi kuwa na timu nzuri ikiwa wachezaji wanadai mishahara yao kwa mwezi na zaidi. Kwa hiyo jambo la kwanza na muhimu ili kuinyanyua klabu ni lazima ujengwe uchumi wa klabu, warudi katika mfumo wa kibiashara. Hili nimelisema siku nyingi.
Kama hamuwezi kurudi katika mfumo wa kibiashara kwa nyakati hizi, haraka sana mtaondoka katika ramani ya soka. Bila kufanya hivyo watabaki tu kuwa klabu kongwe kwa sababu ni miaka minne sasa Simba imemaliza katika nafasi ya tatu na ya nne. Inaondoka katika klabu kubwa na kuwa klabu kongwe.
www.simbadume.co.tz: Wakati ningali kijana mdogo ulipata kuiongoza Simba kwa miezi 6 na ukafanikiwa kuiacha na zaidi ya milioni 80. Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita pesa hiyo ni kiasi kikubwa, uliwezaje kufanya hivyo, njia gani ulizitumia kwa kipindi kifupi kama mtendaji mkuu wa klabu kutengeza chote kile na kukiacha katika akaunti ya klabu, kama kuna ukweli wa hilo.
Michael Wambura: Unajua, ngoja nikwambie kitu kimoja. Tatizo ambalo tunalo katika klabu yetu. Kwanza ieleweke kuwa Simba ina vitenga uchumi, lakini tatizo linalokuja, je, vinafanyiwa uwekezaji? je, mapato yanapoingia yanaingia katika wakati mwafaka? unajua pesa ukiidunduliza, unaingiza leo shilingi 5, kesho shilingi 10 unaweza usiione sana, lakini ukiitafutia utaratibu wa kuingiza na kudhibiti mapato unaweza kupata kitu.
Nikwambie kitu kimoja, sisi tulisajili wachezaki kwa kutumia fedha za ndani za klabu wakati ule (2006.) Hatukutumia hela ya mfadhili hata mmoja. Tulitengeneza na kudhibiti vyanzo vyetu vya mapauo kwa kuangalia vyanzo vilivyo pale klabuni.
Sema tukapata matatizo kidogo baada ya kuanza kudhibiti vyao vya kiuchumi. Ndipo mgogoro ulipoanza pale mimi nikaondoka kwa sababu sasa tulikuwa tunahitaji kujumlisha mapato yote ya Simca. Imeingiza kiasi gani, inajenga nini.
Lakini ikaonekana kuna watu labda hawakutaka hilo. Kikubwa nisingependa kuzumzia mambo yangu binafsi kwa Simba. Unanielewa. Ili nisionekane nawasema watu. Napenda kuzungumza kiujumla ila si mimi kama Michal na kile nilichoifanyia Simba. Hapana, inakuwa kama najitofautisha na uongozi fulani.
Mimi nazungumza ninachokiona na kusema kiendeshwe vipi. Katika karne ya sasa hatupaswi kuendesha mpira kama ilivyokuwa miaka kumi iliyopita. Mpira wa miguu umebadilika, umekuwa mchezo wenye gharama kubwa sana.
www.simbadume.co.tz: Tumekuwa tukiuza wachezaji wetu nje ya nchi kwa zaidi ya milion 100 miaka ya karibuni. Je, nasi tunapaswa kusajili mchezaji hata kwa milion 80 au ni upotezaji wa pesa?
Michael Wambura: Kitu kinaitwa ‘Money for Money.’ Pesa kwa pesa inaangalia, je, huyu mchezaji aliyesajiliwa labda kwa milion 80 uwezo wake unakidhi thamani yake. Hilo ndilo tatizo ambalo tunalo, tunasaji wachezaji utasikia kwa dola 40,000, mara dola 30,000 lakini mwisho wa siku ukiangalia mpira wake uwanjani haulingani na thamani ya milion 80 aliyonayo.
Tatizo kubwa ni wachezaji wetu wengi wanasajiliwa na viongozi badala ya kusajiliwa na makocha. Kiongozi hana upeo wa kufundisha mpira, viongozi wengi wana upeo wa kuangalia mpira. Wakiungalia mpira wanaweza wakauona, lakini kujua mchezaji anatengenezwa vipi hadi anakuwa anachezaji nafasi fulani vizuri ni mwalimu anayejua.
Kweli viongozi bado wanasajili wachezaji na huko ni lazima watoke. Na hili Simba nimeliona sana. Kama viongozi wataendelea kusajili wachezaji wataendelea kuanguka ndani ya uwanja. Tukubali kuna watu wanaweza kufanya kazi fulani.
Simba hadi leo haina Kamati ya utendaji. Wewe umeshawahi kumsikia katibu mkuu wa Simba ni nani? Bado wanaendesha timu kama vile timu ya kijiji. Sababu Simba ilipaswa kuwa na kamati imara ya utendaji ili waweze kufanya mipango ya masoko, waweze kupanga mipango ya maendeleo n.k. Sasa nani anafanya hivyo?
Hawa viongozi wa Simba wa kuchaguliwa kila mmoja ana kazi yake, kwa hiyo wanafanya shughuli za Simba baada ya kumaliza majukumu yao ya kikazi ili kujiingizia kipato chao cha kuendesha maisha ya kila siku. Simba ni taasisi ambayo watu wanapaswa kuamka asubuhi na kuwahi kazini. Unafanya kazi wapi? ‘Nafanya kazi Simba Sports Club.’ Mkurugenzi Simba Sports Club, Meneja Simba Sports Club, Ofisa Simba Sports Club lakini si ilivyo sasa, kuna sijui dereva, karani ni watu wasiozidi watano nadhani ndiyo wameajiriwa Simba hivi sasa.
Bado Simba haijawa klabu inayoongozwa kitaaluma. Leo wanataka kucheza michuano ya kimataifa, ili iweje? Wakati katika ofisi yako umeshindwa kuajiri hata watu watano!
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment