Hassan Kessy Ramadhani atakuwa mchezaji wa Yanga SC kuanzia msimu ujao baada ya mlinzi huyo wa pembeni-namba 2 kumaliza mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu kwenye klabu ya Simba SC. Kessy amesaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara (VPL), timu ya Yanga kwa sababu za kimpira na maslai, pengine hata utulivu kwa maana ndani ya Simba hivi sasa hakuna ‘usalama wa kipaji chake.’
August mwaka jana niliandika makala katika website hii na nilipingana kwa asilimia 100 na mahitaji mapya ya Kessy kwa timu yake ya Simba ili asaini mkataba mpya klabuni hapo. Alihitaji kiasi cha pesa kisichopungua milioni 45 ili asaini mkataba mpya.
Nilikataa hitaji lake hilo na nikashauri ni vyema mchezaji huyo akaachwa aende atakako kwa maana hajafanya kazi yenye thamani ya milioni 25 ambazo alipewa wakati akijiunga na Simba akitokea timu ya Mtibwa Sugar ya kwao Morogoro mwishoni mwa mwezi Disemba, 2014.
Kinachosubiliwa sasa ni muda tu kabla ya Kessy kutambulishwa akiwa na jezi namba 25 yenye rangi za manjano, kijani na nyeusi na kuachana na jezi namba 4 ya ‘Wekundu wa Msimbazi.’ Namba ambayo pia iliwahi kuvaliwa na kiungo, Athumani Idd ‘Chuji’ aliyewahi kuzua utata mkubwa sana wakati alipoachana na Simba na kujiunga Yanga wakati wa usajili wa mwishoni mwa mwaka 2006.
Miaka kumi kasoro miezi 6, Kessy anafuata nyayo za Chuji lakini yeye anaondoka sehemu yake ya sasa katika namna tofauti.
‘SIMBA SI YA BABA YAKO’ ni kauli mbaya kuambiwa, hata kama ilionekana mchezaji huyo anaondoka, kiongozi wa klabu kubwa kama Simba hapaswi kutoa kauli ya namna hii kwa mchezaji wake yeyote.
Kauli hii ilitolewa na mkuu wa kitengo cha habari wa klabu hiyo Haji Manara mbele ya waandishi wa habari wakati klabu ilipoamua kumsimamisha Kessy kutocheza game tano kwa makosa ya kupata kadi nyekundu katika game waliyopoteza 1-0 dhidi ya Toto Africans.
Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Taifa katikati ya mwezi uliopita, Kessy aliondoshwa uwanjani baada ya kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika jaribio lake la kumzuia mshambulizi wa Toto ‘rafiki yake’ Edward Christopher.
Wakati Chuji aliondoka Simba huku aki ‘ikashifu’ Simba kiasi cha kusema ni heri ‘akauze ndimu kuliko kurejea timu hiyo’ baada ya uongozi wa timu chini ya Mzee Hassan Dalali aliyekuwa mwenyekiti wa klabu na katibu wake, Mwina Kaduguda kupigana kwa kila namna kumbakisha mchezaji huyo, lakini Chuji alishikilia msimamo wake wa kutoitaka tena Simba iliyokuwa ikihitaji kuendelea kuwa naye.
Alilazimisha usajili wa kwenda Yanga wakati akiwa na mwaka mmoja zaidi kimkataba na Simba. Huu ulikuwa usajili wa kwanza wa karne mpya ambao uliwaumiza sana mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba.
Manara labda alicheza mpira wakati wake wa ujana, ama anaufahamu kiasi kuhusu historia ya klabu ya Simba, lakini ni asiyeujua vizuri mpira wa Tanzania wala ujuzi wa kumuwezesha kumudu majukumu aliyopewa kama mkuu wa kitengo cha habari.
Kitu pekee ambacho nakiona amefanikiwa sana katika msimu wake wa pili klabuni hapo ni kutengeneza tu marafiki wapya-jambo jingine la muhimu katika maisha. Kiutendaji amefeli na katika orodha ya maofisa habari wanne wa klabu hiyo kuanzia Cliford Ndimbo, Ezekiel Kamwaga, na dada Asha Muhaj, yeye (Manara) ameshindwa kabisa.
Katika safu ya utawala naamini mwenyekiti wa kamati ya usajili ndiye kinara, lakini ndani ya uwanja, Manara ameiangusha timu kwa kiasi kikubwa. Kiukweli niwe mkweli, wakati fulani baada ya Simba kushinda game takribani 7 mfululizo msimu huu nilijenga wasiwasi kwamba huenda wangeshinda ubingwa hasa tofauti ya pointi 7 waliyokuwa wameitengeza dhidi ya wapinzani wao Yanga na Azama FC.
Kuna siku nilizungumza na dereva wa bus la timu ya Tanzania Prisons, rafiki yangu Mwandimo Emmanuel ilikuwa ni baada ya Simba kushinda game 6 mfululizo, akaniuliza, “Kwa nini huwapi Simba nafasi ya kushinda ubingwa?”
Katika maswali rahisi zaidi ambayo nimewahi kukutana nayo, hili la kwanini siipi nafasi ya ubingwa timu ya Simba. “Simba inaendeshwa na genge la wahuni, kikawaida maisha ya wahuni wakati wowote wanakorofishana”, nilimjibu hivyo nikitambua kwamba hata Prisons ingefungwa na Simba lakini hawatashinda ubingwa.
“Simba wako vizuri sana kwa sasa, watazame wanavyopambana”, aliniambia tena maneno ambayo yaliongeza hofu ya wasiwasi wangu.
Wakati ule Chuji ‘alipojihamishia Yanga’ kama mnazi wa Simba niliumizwa sana, niliona jitihada za Kaduguda na Dalali kumpigania mchezaji wao bora kubaki klabuni licha ya kwamba sababu za kimaslai zilimchochea Chuji kusahau kila kitu alichofanyiwa na Simba ambayo ilimsaini kutoka Polisi Dodoma mwishoni mwa mwaka 2005.
Lakini wakati huu nimekuwa mstari wa mbele kuona Kessy akiachwa aondoke zake, lakini si kwa namna ya ‘kumfukuza’ kama alivyofanya Manara. Uongozi wa sasa wa klabu umemfukuza Kessy kwa sababu za kimpira. Ni ajabu kwelikweli, eti mchezaji kufungiwa na klabu yake kwa makosa ya kupiga pasi mbovu katika game au kutokana na makosa ya kimchezo kupata kadi nyekundu katika game!
Nilikataa Kessy kudai milioni 45 kisha 60 ili asaini mkataba mpya na nikasema Simba inaweza kumpa kiasi kikubwa zaidi ya kile anachotaka kama ataisaidia timu ndani ya kushinda kwanza ubingwa wa VPL au kombe la FA ili wapate nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya CAF kwa kuwa haijapata nafasi hiyo tangu mwaka 2012.
Kessy aliyasoma makala yale bila shaka kazi yake aliporejea uwanjani kuanzia mwishoni mwa Januari iliinyanyua sana Simba na kuipeleka hadi kileleni mwa msimu baada ya kupita miaka minne, pia aliisaidia timu yake kutinga robo fainali katika michuano ya FA. Akatangaza dau jipya kutoka milioni 45 mwezi Agosti, 2015 hadi kufikia milioni 60, Juni, 2016.
Kama kawaida nikaandika makala na kusema kwamba mchezaji huyo hana thamani ya milioni 85 ndani ya mwaka mmoja na nusu klabuni hapo. Pia nikasema hata Yanga haiwezi kumsaini kwa zaidi ya milioni 30 kama ataamua kuitosa Simba kwa kuwa tayari inaye Juma Abdul mwenye kiwango cha juu katika beki 2.
Nilimtaka tena kuisaidia Simba ipate ubingwa wa wowote ili wapate tiketi ya CAF, angevuna zaidi. Baada ya pasi yake ya kurudi nyuma kunaswa na mshambulizi wa Yanga, Donald Ngoma kisha kufunga wakati Simba ilipochapwa 2-0, Februari 20, masikini kijana huyu pamoja na mlinzi mwenzake Abdi Banda wakatolewa ‘kafara’ wakati ni wawili hawa waliifanya safu ya ulinzi ya timu hiyo kucheza vizuri na kutoruhusu goli katika game 7 mfululizo.
Banda alilabwa kadi nyekundu na ikumbukwe mchezo wake wa kwanza kurejea uwanjani akiwa katika benchi aligoma kupasha misuli moto alipoambiwa kufanya hivyo na mkufunzi Jackson Mayanja, alikuja kufungiwa na uongozi wa klabu yake kwa nidhamu yake mbaya-Maamuzi sahihi kabisa.
Kessy anaondoka kwa stahili inayothibitisha kauli yangu ya mara kwa mara kwamba, ‘Mafionso’ hawawezi kuinyanyua Simba katika nyakati hizi za sasa. Unamfukuza mchezaji wako bora katika timu kwa kuwa amepata red card au kupiga ‘pasi mkaa’ mfukuzeni na Ajib sasa’.
Kama wewe shabiki sijui mwanachama wa Simba kwanini unawatukana viongozi wa klabu yako hadharani wakati umefurahishwa na namna ya walivyomfanyia Kessy? Wewe naye tatizo la Simba, kama sivyo utakuwa unathibitisha kichwa changu cha habari hapo juu.
Mimi pia nimefurahi kuondoka kwa Kessy, amejitahidi kufikia thamani yake ya milioni 25 aliyoingia nayo Simba, na alijitahidi kuipandisha kabla ya kuangushwa na mafionso. Chuji, 2006 aliondoka na kujiunga Yanga akiwa mchezaji wetu halali, ilituuma sana wanazi wa Simba, mioyoni hadi katika nyuso, ni kwa sababu ya jitihada kubwa zilizofanywa na uongozi, ila sasa Kessy anakwenda Yanga akiwa mchezaji huru huku wanazi wa Simba tukitabasamu nyusoni mwetu huku tukiunguzwa na maumivu ya kumpoteza mchezaji wetu bora, tunapambana na watalawa wetu. Kwanini?
0 comments:
Post a Comment